Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema licha ya wadhifa alionao, akifika kwa mumewe hupiga goti kwa unyenyekevu ili kuimarisha mapenzi na familia.
Samia alisema hayo jana akiwakumbusha wanawake wajibu wao kwenye jamii wakati wa ufunguzi wa tamasha la jinsia linaloendelea kwenye viwanja vya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), jijini Dar es Salaam.
“Nasema haya kwa sababu mwingine anaweza kutoka hapa akasema Makamu wa Rais kasema tupo sawa nyanja zote za jamii, uongo! Hatupo hivyo kwenye nyanja zote,” alisema Samia na kuongeza;
“Pamoja na umakamu wangu wa Rais mbele ya mume wangu nitapiga goti. Sipigi goti kwamba ni inferior (kujishusha) hapana! bali ni huba na mapenzi.”
Pia alizungumzia Benki ya Wanawake na kusema Serikali ina mpango wa kuifufua na kuipa nguvu zaidi baada ya kudorora. Alisema wakati inaanzishwa walitegemea isaidie kukwamua wanawake wengi zaidi kiuchumi.
Katika tamasha hilo, wanawake mbalimbali akiwamo Makamu wa Rais, Spika wa Bunge mstaafu, Anne Makinda, Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya na Balozi Getrude Mongella, walikabidhiwa Tuzo ya Heshima inayolenga kutambua mchango wao kijinsia katika kukuza maendeleo ya Taifa.
Samia alisema mwanamke ana haki sawa na mwanamume kwenye nyanja zote za kijamii na kiuchumi, lakini kuna mila na desturi nzuri ambazo hapaswi kuziacha ili kuimarisha familia yake. “Tuache zile mila potofu na tubebe zile nzuri zinazotufanya tuseme, tusikike na tuonekane. Tushirikiane bila kuacha mila zetu, sifa na desturi nzuri,” alisisitiza.
Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Liundi alisema tamasha hilo linafanyika ili kutafakari na kusherehekea mafanikio, kujadili changamoto na kuweka mikakati ya pamoja ili kuzitatua.