SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 10 Agosti 2017

T media news

Waziri Mkuu: Marufuku Kuweka Bei Ya Tumbaku Kwa Dola Za Marekani

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuanzia sasa ni marufuku kuweka bei ya tumbaku kwa dola za Marekani kwa sababu imechangia kuwaumiza wakulima wa zao hilo.

 Amesema wanunuzi wa zao hilo wana uhuru wa kuweka bei zao kwa dola lakini bei hiyo itafsiriwe kwa shilingi za Kitanzania ili wakulima waweze kutambua bei elekezi tangu mwanzo wa msimu. 

Ametoa kauli hiyo Jumatano, Agosti 9, 2017 wakati akizungumza na wadau wa zao la tumbaku zaidi ya 600 wakiwemo wabunge, viongozi wa dini, chama na Serikali kwenye mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Isike-Mwanakiyungi, mjini Tabora.

 Hivi sasa bei elekezi kwa msimu huu wa tumbaku ni dola mbili za Marekani kwa kilo moja ya tumbaku sawa na sh. 4,400 hadi sh. 4,500 za Tanzania.

 Hata hivyo, Waziri Mkuu ambaye yuko katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani hapa, alionya juu ya mkanganyiko unaowapata wakulima na viongozi wa vyama vya msingi (AMCOS) kwenye kutafsiri bei ya zao hilo kutoka dola za Marekani.

 “Kwa mfano, mkulima anapouza tumbaku anaambiwa kilo zake zina thamani ya dola za marekani 90. Wakati anapokuja kulipwa bei ya shilingi inakuwa imebadilika, kwa hiyo kama aliuziwa wakati thamani ya dola moja ikiwa ni sh. 1,500/- na wakati wa kulipwa imefikia sh. 2,000/- hatalipwa kwa bei ya sasa. Bali atalipwa kwa bei ileile ya zamani jambo ambalo linamuumiza mkulima,”amesema. 

Akiwa hapohapo ukumbini, Waziri Mkuu aliwauliza wawakilishi wa benki za CRDB na NMB bei ya dola moja ni sawa na shilingi ngapi kwa hapo Tabora, alijibiwa kwamba katika benki ya CRDB, dola moja ya Marekani inauzwa kwa sh. 2,200 ilhali katika benki ya NMB, dola moja inauzwa kwa sh. 2,167.