SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 2 Agosti 2017

T media news

Spurs na rekodi mbovu ya Wembley, wataendeleza mazuri ya White Hart Lane?

Na Salym Juma, Arusha

White Hart Lane ulikuwa uwanja wa Tottenham Hotspur tangu mwaka 1899 hadi May 14, 2017. Uwanja huu uliokuwa unapatikana Kaskazini mwa jiji la London ulikuwa na uwezo mdogo wa kuchukua watazamaji 36,284 walioketi vitini. Kwa muda wa miaka takriban 118 Spurs imekuwa ikiutumia uwanja huu kwa mafanikio ya wastani. White Hart Lane hapajawahi kuwa sehemu salama kwa wageni hasa wale wa ndani nikimaanisha vilabu vinavyocheza EPL.

Msimu uliomalizika tuliwashuhudia Spurs wakitoa dozi kwa kila aliyekanyaga nyasi za White Hart Lane isipokuwa kwa vijogoo wa Anfield na mabingwa wa zamani Leicester City ambao kwa pamoja waliambulia sare huku wakiomba mpira uishe. Mabingwa wa EPL, Chelsea waliambulia kipigo huku Mourinho naye akimaliza vibaya pale Hart Lane. Historia iliwabeba sana Spurs hasa pale walipokuwa wanacheza na waingereza wenzao pale Hart Lane.

Alama 55 ndizo ambazo zilipatikana pale White Hart Lane kati ya alama 57 ambazo zilipaswa kukusanywa endapo Spurs wangeshinda kwa 100% nyumbani. Kwa maana hiyo naweza kusema Spurs walishinda kwa 97% nyumbani na hatimaye kuingia kwenye rekodi ya timu zilizowahi kufikisha alama 55 katika michezo ya nyumbani ambazo ni Chelsea, Manchester City na Manchester United ya Alex Ferguson.

Japokuwa Spurs inaungana na Manchester United ya 1995 na Newcastle ya 1996 ambazo zilikusanya zaidi ya alama 50 nyumbani na kushindwa kuupata ubingwa wa EPL ila rekodi hiyo imewasidia kushiriki ligi ya Mabingwa Ulaya. Naamini mashabiki wa Spurs hawafurahishwi na kitendo cha timu yao kuhamisha makazi kwenda Wembley, dimba ambalo litaanza kutumiwa rasmi na Spurs kwenye micchezo yake ya EPL msimu ujao.

Victor Wanyama na Harry Kane ndio waliouaga uwanja wa Hart Lane vizuri kwa kuwafanya Spurs kushinda dhidi ya Man United mnamo Jumapili ya May 14. Siku iliyofuata Wakandarasi waliubomoa rasmi uwanja huo na kuendeleza mpango wao wa kuujenga uwanja mpya. Hali hii iliwafanya FA kuwaruhusu Spurs kutumia Dimba kubwa la Wembley msimu wa 2017-18. Jambo la kujiuliza kwa wanasoka ni je, Wembley unaweza kuwapa mafanikio Spurs?

Tottenham hawajawahi kuwa na rekodi nzuri katika uwanja huu mkubwa kuliko viwanja vyote pale England. Wembley ni uwanja ambao mara kadhaa umekosolewa na makocha, wachambuzi na wachezaji mbalimbali kutokana na ‘Pitch’ yake. Wembley uliwahi kulaumiwa na waingereza kuwa chanzo cha timu yao ya taifa kutokufuzu kwenye michuano ya UEFA Euro 2008. Sir Alex Ferguson, Arsène Wenger, David Moyes na Slaven Bilić wamekaririwa wakiponda ‘pitch’ hii.

Spurs walivunja rekodi ya mahudhurio pale walipocheza dhidi ya Bayern Leverkusen kwenye mechi ya ligi ya mabingwa Ulaya kutokana na kuomba mechi zao za Ulaya za msimu uliopita kuchezwa katika uwanja huu. Mechi nyingi walizocheza Wembley msimu uliopita walifanya vibaya isipokuwa mechi chache walizofanya vizuri ikiwemo ile ya CSKA Moscow. Mechi zingine Spurs iliambulia sare na vipigo katika uwanja huu ambao unachukua Watazamaji 90,000.

Katika mechi 7 ilizocheza Wembley, Spurs iliambulia sare dhidi ya Gent katika michuano ya Europa League huku ikipata vipigo katika michezo mingine. Ikumbukwe Spurs walilala 4-2 dhidi ya mabingwa Chelsea katika mchezo wa nusu fainali ya FA. Rekodi hii inawatia mashaka mashabiki wa Spurs licha ya kuwa na rekodi ya kuujaza Uwanja kwa mahudhurio ya 85,000 pale walipocheza dhidi ya Leverkusen. Kuna kila sababu ya kuwa njiapanda kuhusu uwanja huu kwa Spurs.

Wembley una ukubwa wa mita 105 {urefu} na mita 69 {upana} tofauti na White Hart Lane ambao una urefu wa mita 100 na upana wa mita 66. Vipimo hivi vina ‘impact’ kubwa kwenye soka hasa endapo kama uwanja uliokuwa unautumia awali una vipimo vidogo. Barcelona wamekuwa wakivisumbua Vilabu vingi kutokana na Vipimo vya uwanja wao. Nawaona Spurs ‘waki-struggle’ kupata ushindi katika michezo yao katika uwanja huu.

Kwa kuhitimisha, Spurs itafaidika na mauzo ya tiketi kutokana na ukubwa wa Uwanja huu ambao ulianza kutumika mwaka 2007. Spurs chini ya Levy wamekuwa wakibana matumizi ili waweze kukamilisha ndoto ya kumiliki uwanja wao ambao huenda ukakamilika mwaka 2018. Pia pesa itakayotumika kwenye mauzo ya tiketi itatumika kwenye dirisha la usajili msimu ujao. Inawezekana Spurs wakapata faida nje ya uwanja ila kwa ndani bado ni kiza.