Huenda jana Agosti 6 ilikuwa ni siku ambayo Rais Dkt Magufuli alionyesha kukasirishwa sana na baadhi ya wasaidizi wake aliowateua, baada ya kuona hawafanyi kazi kama inavyotakiwa, na hivyo kuisababishia matatizo serikali yake.
Rais Magufuli jana alisema kuwa baadhi ya mawaziri ni wapumbavu kwa kushindwa kuchukua maamuzi ya haraka kuhakikisha mita za kupimia mafuta (flow meters) zinafungwa katika Bandari ya Tanga na Dar es Salaam ili serikali ijue ni kiasi gani cha mafuta inachoingiza nchini.
Rais aliyesema hayo wakati akifungua awamu ya kwanza ya mradi wa kituo cha matanki ya mafuta cha GBP kilichopo katika eneo la Raskazone Mjini Tanga ambacho kina uwezo wa kuhifadhi lita Milioni 122.6 na ambacho kinatarajia kupanuliwa hadi kufikia lita Milioni 300 ifikapo katikati ya mwaka ujao.
Rais Magufuli alielezea kutoridhishwa kwake na kusuasua kwa mchakato wa ununuzi wa mita za kupimia mafuta yanayoshushwa kutoka kwenye meli (Flow Meter) na ametaka Wizara zinazohusika katika mchakato huo kununua mita hizo haraka ili mafuta yanayoingia nchini yapimwe kwa usahihi na kukusanya kodi stahili.
“Japokuwa maneno yangu yanaweza kuonekana na makali, lakini wakati mwingine ni bora ukweli usemwe. Ni tarikabini mwaka mmoja sasa tangu Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) alipoagiza kufungwa kwa mita za kupimia mafuta bandarini, lakini hadi sasa hakuna kilichofanywa,” alisema Rais Magufuli.
Kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma, Rais alisemaa zabuni ingeweza kutangazwa ndani ya siku 45, lakini mwaka unakaribia kufika na zabuni hazijatangazwa tangu Waziri Mkuu walipotoa maagizo hayo.
“Nilipoingia madarakani, niliahidi kupambana na rushwa na ufisadi na ninahisi kuna kitu hapa. Ninawaonya kuwa, hakuna atakayesalia.”
Baada ya kusema hayo, Rais Magufuli alimuagiza waziri mwenye dhamana, kukaa na wadau na kuhakikisha mita hizo zinafungwa katika bandari za Dar es Salaam na Tanga haraka iwezekanavyo.
“Nilipokuwa nagombea, niliahidia kusema ukweli na nitaendelea kufanya hivyo. Najua kuna watu wananikosoa lakini mimi sijali,” alisema Rais huku wananchi wakimshangilia.
Mbali na wizara hiyo, Rais Magufuli aliionya EWURA endapo itachelewesha ufungwaji wa mita hizo, huku akisema kwamba, baadhi ya maafisa wa EWURA wamekuwa wakipandisha bei ya mafuta yanayoingizwa kupitia bandari ya Tanga.
Rais Magufuli ambaye bado yupo mkoani Tanga, leo anatarajia kuhitimisha ziara yake ya kikazi ya siku 5 mkoani humo.