Tanzania na Misri zimekubaliana kukuza ushirikiano katika maeneo mbalimbali ya kibiashara na kiuchumi pamoja na nchi ya Misri kuongeza fedha katika hospitali ya Muhimbili ili iwe inafanya operesheni ya figo.
Akizungumza jijini Dar es salaam baada ya mazungumzo yake na Rais wa Misri, Abdel Fattah Al Sisi, Rais Magufuli amesema wamekubaliana kuboresha sekta ya kilimo afya na biashara.
“Sasa tukuze biashara katika nchi hizi mbili, tumezungumza kwa mfano Tanzania ni wa pili kwa kuwa na mifugo mingi na nchi ya Misri inahitaji nyama tumekubaliana kuendelezana katika masuala ya kilimo ikiwepo kwenye masuala ya irrigation(umwagiliaji) ambayo ndio yameliendeleza taifa la Misri tangia miaka na miaka na miaka,” alisema Rais Magufuli.
“Kwahiyo wameamua hiyo Teknolojia kushirikiana na Tanzania katika masuala hayo lakini pia tumeahidi kushirikiana katika masuala ya afya wamekuwa wakitusaidia kwa baadhi ya wataalam na vifaa katika hospitali ya Dar es salaam Muhimbili pamoja na hospitali ya Zanzibar sasa wameamua kupanua zaidi huo wigo vizuri huo wigo na sasa wameamua wataongeza fedha kuwa sasa hospitali ya Muhimbili itakuwa inafanya operesheni ya figo pamoja na masuala mengine ambayo ni muhimu kabla haijafika 2020.”