SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 13 Agosti 2017

T media news

Maagizo ya Waziri kwa mrithi wa Jamal Malinzi TFF

 Na Genofeva Matemu – WHUSM

Uongozi mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) umetakiwa kufikia Januari mwakani kuwajibika kama mashirika mengine ya mpira wa miguu duniani yanavyowajibika kuchapisha taarifa ya mapato na matumizi kwenye magazeti ili wananchi wapate fursa ya kufahamu namna fedha zinavyopatikana na jinsi zinavyotumika katika kuboresha na kuendeleza usimamizi bora wa soka nchini.

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe wakati wa kufunga Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na katika ukumbi wa St. Gasper Mkoani Dodoma.

Aidha Mhe. Mwakyembe amewapongeza viongozi wapya waliochaguliwa kuiongoza TFF kwa muda wa miaka minne kwa kuwataka kufanya kazi kwa ushirikiano na kwa pamoja katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku huku akiwapongeza washiriki wote waliothubutu kuwania uongozi katika nafasi mbalimbali wakati wa uchaguzi Mkuu wa TFF wa mwaka huu.

Kwa upande wake Rais mpya wa TFF Bw. Wallace Karia amewaahidi wapiga kuwa wake kufanya kazi kwa weledi wa hali ya juu kwani nafasi aliyopewa na wajumbe hao kwa kumuamini ni deni ambalo atalilipa kwa kuleta mafanikio makubwa katika mchezo wa soka.

Bw. Karia amesema kuwa furaha waliyonayo viongozi wote waliochaguliwa kuiongoza TFF kwa muda wa miaka minne iende kuwa furaha ya kazi kwa kufanya yale watanzania wanatarajia kutoka kwao.


Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza na wajumbe wa TFF (hawapo pichani) baada ya kutangazwa na kuapishwa kwa viongozi wapya wa TFF Mkoani Dodoma.

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Bw. Wallace Karia akitoa neno la shukrani kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa TFF kumwezesha kushika nafasi ya urais, wakati wa Mkutano Mkuu wa TFF uliofanyika katika Ukumbi wa St. Gasper Mkoani Dodoma.

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) akiteta na Makamu wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Bw. Michael Wambura (kushoto) baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa TFF uliofanyika jana katika ukumbi wa St. Gasper Mkoani Dodoma.