August 16, 2017 Real Madrid ilibeba kombe la Spanish Super Cup baada ya kuifunga Barcelona 2-0 kwenye mechi ya marudiano na kufanya ushindi wa jumla kuwa 5-1 kwani tayari Barca walichapwa 3-1 kwenye uwanja wao wa nyumbani wakati wa mchezo wa kwanza.
Mbali na kipigo cha 2-0, Madrid walitawala mpira muda wote wa mchezo huo na kuwapoteza kabisa Barca jambo ambalo halijazoelekwa siku za hivi karibuni. Barcelona imeshapoteza mechi nyingi dhidi ya Madrid lakini si kwa kupoteana uwanjani, mjadala ndio upo hapa.
Baada ya vipigo viwili mfululizo kwa Barca wadau wengi wa soka wamekuwa wakihusisha vichapo hivyo na kuondoka kwa Neymar ambaye amejiunga na PSG.
Mimi Shaffih Dauda nipo tofauti kidogo kimtazamo na wale wanaoamini kufanya vibaya kwa Barca ni matokeo ya kuondoka kwa Neymar Jr.
Barcelona imeanza kupoteza makali yake tangu misimu mitatu nyuma, lakini imekuwa ikibebwa na uwezo wa wachezaji binafsi na sio timu kwa ujumla wake.
Matokeo ambayo tumeyapata kwa hii miaka miwili au mitatu yametokana na viwango binafsi vya wachezaji watatu wa mbele Messi, Suarez na Neymar (MSN) ndio wamekuwa wakizungumzwa sana tofauti na miaka ya nyuma ambapo ilikuwa inazungumzwa timu.
Ilikuwa ukizungumza ubora wa Barca basi unazungumzia style yao ya uchezaji kama timu, namna wanavyomiliki mpira, jinsi wanavyourudisha mpira kwenye himaya yao sekunde chache baada ya kuupoteza, kasi na wanavyotanua uwanja.
Ukiangalia misimu miwili nyuma hadi huu uliomalizika, utagundua Barcelona imekuwa ikibebwa na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja na kuiweka mahali ilipo sasa.
Kwa wale wanaoifuatilia vizuri Barca, historia yao ya nyuma wakati wanapambana miaka ya 1990 walipompata Johan Cruyff kama kocha ni kipindi ambacho Barca ilifanya mapinduzi makubwa ya kikosi na kupata ‘the dram team.’
1992 wakachukua ndoo ya UEFA Champions League chini ya Cruyff, baada ya hapo Cruyff akaondoka akiwa ameshachukua mataji manne ya La liga mfululizo.
Kuanzia mwaka 2003 alipoingia Joan Laporta kama Rais wa timu, alifanya mapinduzi makubwa akiwa Rais wa klabu. Alikuja na falsafa yake na Barcelona anayoitaka yeye, itakayokuwa na mbinu sambamba na soka la style ya Cruyff.
Akaitengeneza Barcelona kwa msingi wa kuwaandaa wachezaji wake kutoka kwenye academy yao wenyewe. Hapa ndipo akamchukua Frank Rijkaard anakuwa kocha, uwekezaji na nguvu kubwa ikawekwa kwa vijana kama Iniesta na Xavi na kuwaongeza wachezaji wenye majina kama Ronaldinho, Giuly, Eto’o, Edmilson na wengine.
Barcelona hiyo ikashinda tena ubingwa wa Champions League 2006 na mataji ya La liga. Akaondoka Rijkaad akampisha Pep Guardiola na hapa ndio balaa lingine likaanza.
Mwaka 2010 kwenye uchaguzi, Laporta akaangushwa na Sandro Rossel ambaye akaja pia na falsafa yake. Wakati huu Barca walikuwa wakisimama kwenye kile wanachokiita ni utamaduni wao wa ‘kikatalunya’.
Barcelona walikuwa hawaweki matangazo ya biashara kwenye jezi zao, waliweka tangazo la Unicef kama sehemu ya kurudisha kwa jamii lakini hawakuwa wakipata pesa au faida kutokana na matangazo ya kwenye jezi.
Baada ya Rossel kuingia akasema Laporta alikuwa anaiongoza vibaya Barca na kuitia hasara. Baadae Rossel akapata kesi na kuhukumiwa jela akaiacha Barca mikononi mwa Josep Maria Bartomeu ambaye alikuwa makamu wa Rais.
Sasa ukiangalia tangu alipotoka Laporta ambaye ndiye aliyetengeneza misingi ya Barcelona ambayo tumeiona ikifanya vizuri miaka ya hapa katikati sasa hivi Barcelona inaendeshwa kwa utamaduni mpya wa kununua sana wachezaji na kutowapa kipaumbele wachezaji wa La masia.
Angalia leo hii wanamtambulisha mchezaji kama Paulinho mwenye miaka 29, hii imezua mijada mikubwa kwa mashabiki wa Barcelona ambao wanaamini mchezaji kama Paulinho si wa aina yao.