Furaha kubwa iliwajaa mashabiki wengi na watanzania kwa ujumla kufuatia ujio wa klabu ya Everton ya nchini Uingereza ambapo leo itashuka dimbani kumenyana na Gor Mahia ya Kenya mchezo utakaopigwa katika uwanja wa taifa Dar.
Miongoni mwa wachezaji waliowavutia watu wengi mara tu baada ya kutua Tanzania ni mshambuliaji wa Uingereza na aliyekuwa mchezaji wa Manchester United, Wayne Rooney.
Furaha hii pia ilimkuta Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassa ambapo jana usiku alipata nafasi ya kushiriki chakula cha usiku na wachezaji hao pamoja na wageni wengine walioambatana nao.
Usiku huo Makamu wa Rais alitoa siri pengine hakuna mtu aliyekuwa akiifahamu ambapo alisema yeye ni shabiki wa mpira wa miguu na anaipenda Manchester United.
“Wayne Rooney alisababisha nikaipenda na kuishabikia Manchester United, lakini sasa sijui nitafanyaje kwa sababu amerejea Everton,” alisema Makamu wa Rais.
Akijibu hilo, Wayne Rooney alisema kuwa, kuwepo kwake Tanzania limekuwa ni jambo la furaha kwake na anaamini kuwa Makamu wa Rais ataweza kuishabikia Everton.
Huu unaonekana kuwa mtihani kwa Makamu wa Rais kwani kama tayari anaipenda Manchester United, ni kivipi anaweza kuhamia Everton? Lakini baadhi husema kuwa, timu sio kabila kwamba huwezi kuhama.
Everton imekuja nchini ikiwa ni ziara iliyoandaliwa na wadhamini wao Sportpesa ambayo ni kampuni ya kubashiri kutokea nchini Kenya.