SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 15 Julai 2017

T media news

Wagombea CCM Kibiti Washindwa Kuchukua Fomu....Kisa....

Wakati hali ya wasiwasi ikizidi kushamiri kwa wakazi wa wilaya za Kibiti na Rufiji juu ya usalama wa maisha yao kutokana na kuendelea kwa matukio ya mauaji, hofu hiyo bado imetanda miongoni mwa wanachama wa CCM wanaohofia kuchukua fomu za kuwania uongozi ngazi ya matawi na shina.

Akizungumza na gazeti la Mwananchi kwa njia ya simu, Katibu wa Siasa na Uenezi wa chama hicho katika wilaya hizo, Mussa Mnyeresa amesema sababu za wanachama kususa kuchukua fomu hizo hasa ngazi za tawi, shina na  nafasi nyingine ni mfululizo wa matukio ya mauaji yanayoendelea katika wilaya hizi.

Amesema katika wilaya ya Kibiti, kata za Mjawa, Ruaruke na Mchukwi yanaongoza kwa wanachama wa chama hicho kutochukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Aidha amesema katika wilaya ya Rufiji uchukuaji fomu za nafasi za uongozi Tarafa ya Ikwiriri yenye Kata tatu za Umwe, Mgomba na Ikwiriri napo zoezi la uchukuaji fomu wa nafasi hizo si la kuridhisha.

Mnyeresa amesema hadi sasa kasi ya uchukuaji fomu hizo katika kata hizo bado ipo chini huku viongozi wa chama hicho wakiendelea kuwahamasisha wanachama wa chama hicho wachukue fomu.

Amesema uongozi wa chama hicho ngazi ya wilaya hizo ambazo awali ilikuwa ni wilaya moja tayari umepeleka taarifa za wanachama kwenye baadhi ya maeneo kutochukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali wakihofia usalama wao.

Akizungumza juu ya wanachama kuchukua fomu za uongozi Ngazi ya Tawi na Shina katika wilaya ya Kibiti, Katibu wa chama hicho wilayani hapa, Zena Mgaya amesema hali ya uchukuaji fomu kwenye ngazi hizo hairidhishi.

Zena alisema katika ngazi za uongozi za kata na wilaya hali inaridhisha na wanachama wamehamasika kuchukua fomu hizo.

Amesema hadi sasa kati ya kata 16 zinazounda wilaya ya Kibiti, tayari wamepokea fomu za kata 10 za wagombea wa nafasi za tawi na shina.

Amesema kwa upande wa nafasi za uongozi wa ngazi za kata na wilaya, bado wanachama wanaendelea kuchukua fomu na kuzijaza.

Zena amesema pamoja na kuwepo hofu ya mauaji kwa wananchi na wanachama wa chama hicho, bado mwitikio ni mzuri zaidi kwenye nafasi za kata na wilaya.

Akizungumzia wanachama wa chama hicho kutochukua fomu hasa za ngazi ya tawi, mmoja wa wanachama wa chama hicho, ambaye pia ni Diwani Kata ya Mtawanya, Malela Tokha amesema ni vyema uongozi wa chama hicho ngazi ya taifa ukayafanyia kazi maombi ya wanachama wa chama hicho waliyoomba uchaguzi huo usogezwe mbele.

Amesema hali hiyo itaepusha chama hicho kupata viongozi wasiokuwa na sifa na uwezo na kuzidi kukidhoofisha chama kwa kuwa wakati huu wanachama wenye uwezo wengi wao wanaogopa kuchukua fomu za kugombea nafasi za uongozi.