Hali ya ulinzi mkali ilianza kuonekana juzi wakati wa maandalizi ya mwisho wa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) baada ya magari mengi ya vyombo vya ulinzi na usalama kutembelea eneo hilo yakiwa na watu waliovalia suti na miwani huku wakikagua nyumba zilizo jirani na maeneo ya viwanja hivyo vya sabasaba.
Ulinzi mkali uliongezewa jana asubuhi wakati wa maandalizi ya jukwaa na uwekaji viti kwani wanausalama walionekana wakiwa wametanda katika eneo hilo na kila mtu aliyetaka kuingia katika eneo la shughuli alipekuliwa kwa vifaa maalum vya kielektroniki kubaini kama mtu amebeba kifaa chochote kinachoweza kuwa silaha.
Sehemu kubwa karibu ya jukwaa kuu ilikuwa imezungushiwa uzio ambapo hakuna mtu aliyeweza kuingia bila ya kukaguliwa na kulikuwa na wanausalama wakilinda kila kona ya uwanja huo na maeneo yote ya jirani ambapo wanausalama kadhaa walionekana katika majengo yote ya ghorofa yaliyo karibu na viwanja hivyo wakiwa na darubini wakiangalia hali inavyoendelea kwa muda wote ambao kiongozi huyo mkuu wa nchi alikuwepo eneo hilo.
Kabla ya Rais Magufuli kuingia uwanjani hapo, waliongezeka wanausalama zaidi na askari wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia, maarufu kama FFU wakiwa wamevalia mavazi maalum na bunduki za kisasa na kuzunguka uzio uliowekwa.
Askari hao walionekana kufanya kazi yao kwa ustadi mkubwa kwani hawakugeuka kufuatilia kilichokuwa kikiendelea viwanjani hapo kama wananchi wengine bali walikuwa wakitekeleza majukumu yao ya kikazi. Wananchi waliokuwepo walionekana kuwa na utulivu muda wote na wengi walikuwa na shauku ya kumwona na kumsikiliza Rais na wakati mwingi alipokuwa akihutubia walimshangilia.
Wengi wanajiuliza iwapo ulinzi wa hali ya juu kiasi hiki ambao unaweza kuufananisha na ulinzi tulioushuhudia tulipotembelewa na Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama ndio ulinzi wa kawaida kwa Rais Magufuli ama kulikuwa na taarifa za kiusalama kwamba yawezekana wanaoendesha vitendo vya mauaji ya viongozi katika Wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji wanaweza kujaribu chochote cha kumdhuru Rais wetu.
Yote kwa yote, timu hiyo ya wanausalama ilitia fora na kuwa moja ya vivutio vikubwa ambavyo wananchi waliohudhuria katika viwanja hivyo walivishuhudia kwa muda wote ambao Rais Dkt. Magufuli alikuwa viwanjani hapo kwa sherehe rasmi za uzinduzi wa maonesho hayo yatakayodumu mpaka tarehe 13 mwezi huu.