Mwili wa mtu ambaye hajafahamika umeokotwa katika bwawa la maji lililopo Mtaa wa Nkende Shuleni katika Halmashauri ya Mji wa Tarime.
Hili ni tukio la tatu la watu kuuawa kisha miili yao kutupwa kwenye mabwawa ya maji katika kipindi cha miezi sita iliyopita. Hivi karibuni, mwili wa kijana ambaye alikuwa dereva wa bodaboda ulikutwa ukiwa umetupwa katika eneo hilo hilo.
Kamanda wa Mkoa wa Polisi Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe, amethibitisha kuokotwa kwa mwili huo na kubainisha kuwa Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi ili kuwabaini watu wanafanya mauaji hayo.
Chareles Kisege, ambaye ni mwenyekiti wa mtaa wa Nkende Shuleni na James Nyangai mwenyekiti wa mtaa wa Kimusi, wamesema matukio hayo yamezusha hofu miongoni mwa wananchi wanaoishi katika maeneo hayo.
Wamitaka serikali kuchukua hatua za haraka kuwadhibiti wauaji hao.
Licha juhudi za wananchi kutaka kuuopoa mwili huo, zoezi hilo limekuwa zito na gumu kutokana na kukosa zana.
Hata hivyo, mwenyekiti wa chama cha waendesha bodaboda wilayani hapa, Samwel Kegoye, amesema ingawa taarifa zinaonyesha kuwa mtu huyo aliyeuawa ni dereva wa bodaboda, wao badoi hawajapata taarifa hizo rasmi.