Wabunge sita wa Chadema usiku wa kumkia leo wamehojiwa na polisi kwa tuhuma za kumshambulia Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Juliana Shonza.
Akizungumza na Mwananchi Jumatatu usiku, mwenyekiti mwenza wa wabunge wanaounda umoja wa katiba (Ukawa) James Mbatia amewataja wanaoshikiliwa kuwa ni Mbunge wa Mlimba Suzan Kiwanga, Saed Kubenea(Ubungo), Pauline Gekul (Babati Mjini), Frank Mwakajoka (Tunduma), Joseph Selasini (Rombo) na Cecilia Pareso (Viti Maalum).
Hadi saa 5.00 usiku wabunge hao bado walikuwa wakiandika maelezo katika kituo cha polisi. Wabunge hao ni kati ya wabunge wanane waliotajwa na Spika wa Bunge Job Ndugai alipokuwa akiahirisha kikao cha bunge jioni kuwa wanatuhumiwa kumshambulia Shonza.
Wabunge wengine waliotajwa katika sakata hilo lililotokea Jumatatu mchana mchana katika lango la kuingilia jengo la utawala ni Devotha Minja (Viti Maalum) na Cecil Mwambe (Ndanda).
Hata hivyo James Mbatia alipohojiwa na Mwananchi Saa 5.45usiku alisema kuwa wabunge hao waliachiwa kwa dhamana baada ya mahojiano na kutakiwa kurud polisi Jumanne Saa 3 asubuhi.
Hata hivyo Mbatia ameshangazwa na kitendo cha kutajwa kwa Mwambe ambaye amesema hii ni wiki ya pili hayupo mjini Dodoma.
“Mimi nilikuwa msimamizi wa kambi yetu, Mwambe aliniaga tangu wiki mbili zilizopita anaenda jimboni na hajarudi sasa tunashangaa kutajwa alikuwepo wakati wa tukio,” amesema.
Wabunge hao walidakwa mmoja mmoja na askari waliokuwa wamevalia mavazi ya kiraia (askari kanzu) wanaolinda bunge.
Mwananchi ilishuhudia askari hao wawili wa kike na wa kiume wakiwafuata Kiwanga na Kubenea mara baada ya bunge kuahirishwa na kutoka nao nje ya viwanja vya bunge.
Kukamatwa kwa wabunge hao kulifuatia Shonza kwenda kushtaki kwa Ndugai naye kutoa kibali cha kukamatwa kwa wabunge hao.
-MWANANCHI