SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 9 Juni 2017

T media news

Ngasa anaweza kendelea kuibeba Yanga, lakini ni usajili wa Lwandamina au kina Mr. Kazinyingi?

Na Baraka Mbolembole

USAJILI wa Mrisho Ngasa kutoka Mbeya City FC na kujiunga Yanga SC unaweza ‘kufurahiwa’ wanachama/wapenzi wengi wa mabingwa hao wa kihistoria Tanzania Bara, lakini kwa ‘jicho langu la tatu’ naamini, Ngassa hawezi kuleta kipya chochote katika kikosi cha kocha Mzambia, George Lwandamina.

Ngasa licha ya kuwahi kuzichezea Azam FC (2010-2012), Simba SC (2012/13) katika soka la Tanzania kiungo huyo mshambulizi amejitambulisha kama ‘mchezaji hasa wa Yanga’ ambayo amewahi kuichezea kwa mafanikio makubwa katika vipindi viwili tofauti miaka ya nyuma.

NGASA WA SASA SI YULE WA 2006

Wakati anasajiliwa Yanga kwa mara ya kwanza akitokea Kagera Sugar FC mwishoni mwa mwaka 2006, Ngasa alikuwa bado ‘kijana mdogo’ huku kasi yake uwanjani ikiwafanya mabeki wa timu pinzani kupata wakati mgumu kila walipokabiliana naye.

Alikuwa akikimbia vizuri huku akikokota mpira, alikuwa na kasi ya kukimbilia pasi ‘iliyopenyezwa’ katika eneo la wazi. Si hivyo tu Ngasa alikuwa akicheza kwa ‘kuhaha’ eneo lote la mbele huku akiichezesha timu, kutengeneza nafasi za magoli, kupiga pasi za mwisho na kufunga magoli.

Ni wapinzani wake tu ambao hawakupenda kumtazama Ngasa lakini kwa ‘watu wa Yanga’ hadi sasa hawaamini kama timu yao imewahi kupata mchezaji bora na mwenye mapenzi ya dhati kwa timu yao kama Ngasa.

Ndiyo, Ngasa ni kati ya wachezaji bora waliopata kutokea katika soka la Tanzania ndani ya karne hii, lakini kwa sasa yuko mbali na kiwango chake kile ambacho alikionesha katika michuano ya CHAN 2009 Ivory Coast.

Majeraha na maisha ya nje ya uwanja yamepunguza kasi ya Ngasa. Sasa hakimbii mara kwa mara na mpira na amekuwa ‘mvivu’ kukimbilia pasi za kupenyeza ambazo amekua akipigiwa. Ngassa wa sasa ‘anajitafutia kieneo’ kidogo cha kukimbia na kujaribu kufanya ufundi wake lakini bado si mahiri katika upigaji wa pasi za mwisho wala ufungaji.

Wakati, Saimon Msuva akiwa bado hajafikia kiwango alichokionyesha Ngasa miaka ya 2007 hadi 2015, Ngasa wa sasa kwa upande wake anahangaika kufikia walau nusu tu ya uwezo wa sasa alionao Msuva.

SI USAJILI WA LWANDAMINA

Na kama ni usajili wa Mzambia huyo ni ishara ya ‘anguko’ la Yanga. Usajili wa Mzambia, Justine Zulu umekuwa na matokeo hasi hadi sasa na kwa mchezaji anaye ‘umia umia’ kama kiungo huyo wa kati bila shaka, Lwandamina alifanya makosa ya kumsaini mchezaji huyo. Emmanuel Martin alionwa na macho ya Lwandamina mara moja tu wakati Yanga ilipocheza na JKU katika mchezo wa kirafiki. Kiungo huyo mshambulizi wa pembeni hajaongeza kipya katika kikosi cha Yanga na Lwandamina ‘alibebwa’ na kikosi kilichosukwa na Mholland, Hans van der Pluijm.

Hans alikataa kumsaini Ngasa mara baada ya mchezaji huyo kuvunja mkataba wake wa miaka mitano na Free State Stars ya Afrika Kusini, Septemba 2016.

Hans aliondolewa Yanga huku sababu mojawapo ikiwa ni kukataa urejeo wa mara ya tatu wa Ngasa klabuni hapo. Na alisema wazi anatazama zaidi maendeleo ya Yanga ndani ya uwanja na ukuaji wa vijana kama Msuva, Deus Kaseke, Juma Mahadhi na Geofrey Mwashuiya.

Najiuliza kipi kimemvutia Lwandamina hadi kutaka kumsaini ‘Ngasa mkaa benchi’ katika kikosi cha City, au ni usajili wa ‘kina-Mr. Kazinyingi’ unarejea Yanga? Hassan Kabunda, Rafael Daud walifaa zaidi kuchukua nafasi ya Ngasa.

NGASA ANAWEZA KUENDELEA KUIBEBA YANGA

Kama yeye mwenyewe ataitumia nafasi hii ‘inayoweza’ kuwa ya mwisho kwake kuvaa jezi ya Yanga, jambo la kwanza ahakikishe anapambana kuyashinda majeraha yake ya mara kwa mara.

Akiwa fiti walau asilimia 70 anapaswa kupambana kuingia katika kikosi cha kwanza chenye washambuliaji watatu au wawili. Ngasa wa sasa anaweza kukupa faida kama utamuondolea majukumu ya kukimbiza timu na kumpa nafasi ya kucheza karibu na goli.

Ngasa anajua kufunga hivyo si ajabu akaendelea kuchanua katika timu ya ‘ndoto zake’ na kujikita katika mioyo ya wana Yanga.

Karibu tena Yanga, Mrisho Ngasa hata kama ni urejeo wa sajili za Mr. Kazinyingi kuna kundi kubwa la mashabiki linaunga mkono usajili wako, kazi kwako na Lwandamina. Mashabiki wa Yanga wana mapenzi ya dhati ila ‘wana kinai’ haraka.