Shirika la Umeme, Tanesco limesema hakuna gharama zozote zinazotozwa kwa mteja anayetaka kubadilishiwa tarifu kutoka juu kwenda chini...
Akizungumza na wanahabari mwishoni mwa wiki iliyopita, Kaimu Meneja Masoko wa Shirika hilo nchini, Mussa Chowo alisema mteja anayetaka kubadilishiwa tarifu hatakiwi kutozwa gharama zozote.
Alisema wateja wa kawaida kabisa wanatakiwa kutumia tarifu namba nne ambayo ni lazima matumizi yake ya umeme yasizidi uniti 75 kwa mwezi na gharama za kila uniti ni sh. 100.
Kundi ya la pili ni wateja wa tarifu ya pili ambao hutumia umeme wa uniti sifuri hadi 1,750 ambao hulipia sh. 292 kwa uniti bila kodi ya ongezeko la thamani (VAT).
“Tunawaomba wananchi kote nchini kuhakikisha hawachajiwi (hawatozwi) malipo yoyote ikiwa wanataka kubadilishiwa tarifu," alisema Chowo.
"Yeyote atakayetendewa hivyo basi ajue ni kosa la jinai na atoe taarifa kwa ajili ya hatua stahiki kwa aliyetenda kosa hilo.”
Alisema Tanesco imeshatoa elimu kwenye baadhi ya mikoa hapa nchini hasa ile iliyopata miradi ya Rea, lengo likiwa ni kuwapa wananchi elimu ya kutosha juu ya haki zao na matumizi sahihi ya umeme ili kuepuka gharama.