SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 4 Mei 2017

T media news

Mwakyembe Apiga Marufuku Magazeti Kusomwa Redion na Katika Television

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison G. Mwakyembe (Mb), jana tarehe 03 Mei, 2017 alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, jijini Mwanza. 

Mhe. Mwakyembe alipokea hotuba na matamko kutoka kwa Mabalozi na wawakilishi wa taasisi mbalimbali zikiwemo Umoja wa Mataifa, UNESCO, Umoja wa Nchi za Ulaya, Baraza la Habari Tanzania, Mfuko wa Vyombo vya Habari na Klabu za Waandishi wa Habari Mikoani.

Katika hotuba yake, Mhe. Mwakyembe aliwahakikishia Wanahabari kwamba Serikali itaendelea kuweka mazingira bora, salama na wezeshi ili kuilea na kuikuza tasnia ya habari. 

Mwakyembe aliwakumbusha wanahabari kwamba Serikali tayari ilishakamilisha utungaji wa Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa na Sheria ya Huduma za Habari ambazo zote zimekamilika mwaka 2016, hivyo wazizingatie katika utendaji kazi wao.

 Mwakyembe pia aliwasihi wanahabari kuwa wakweli na kuzingatia misingi na maadili katika kazi zao. "Mlinzi wa kwanza wa Waandishi wa Habari ni Mungu, Mlinzi wa Pili ni Kalamu ya Mwandishi mwenyewe hasa anapozingatia maadili ya kazi yake," alisisitiza Mhe. Mwakyembe. 

Mhe. Mwakyembe alielekeza Idara ya Habari ya Habari-Maelezo kuwa na utaratibu wa kukutana na Wahariri wa Vyombo vya Habari mara kwa mara ili kubadilishana mawazo na kutoa taarifa sahihi za Serikali.

Aidha, Mhe. Mwakyembe aliwashauri wanahabari kuzichukulia taarifa za mitandao ya kijamii kama "tetesi" ambazo huitaji utafiti kabla ya kuzitumia. 

Mhe. Mwakyembe alivitaka vituo vyote vya runinga na redio viwe vinasoma vichwa vya Habari tu vya magazeti na visisome habari hizo kwa kina mpaka kurasa za ndani za magazeti kwa kufanya hivyo kunaathiri biashara za magazeti.

Mhe. Mwakyembe pia alitumia fursa hiyo kusisitiza kuwa hakuna uhuru usio na mipaka hivyo wanahabari watimize  wajibu wao bila husda wala mawaa na kuzingatia misingi ya sheria na taaluma. 

Aidha, Mhe. Mwakyembe aliwaahidi wanahabari wote ushirikiano wa karibu kwa wakati wote na aliweka utaratibu wa kukutana nao mara kwa mara ili kutazitatua changamoto zinazowakabili.