MKUU wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, amemwagiza Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ukerewe kumkamata Diwani wa Kata ya Bwisya, Dismas Busanya (CCM) pamoja na aliyekuwa mtendaji wa kata, Ladslaus Mabagala, kutokana na kuhusika na ubadhirifu wa Sh milioni 6 za ujenzi wa nyumba ya watumishi.
Akizungumza juzi akiwa Kisiwani Ukara, ambako alikwenda kukagua miradi ya maendeleo, Mongela alisema ameshangazwa na taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali kueleza pia kuwa nyumba wa watumishi iliyoanza kujengwa mwaka 2012 imekamilika, wakati haijaezekwa hata paa.
Alisema nyumba hiyo ambayo ilijengwa kwa Sh milioni 17 ilikuwa haijawekewa lenta wala kuezekwa, lakini katika taarifa zao wamekuwa wakieleza kuwa zikamilika na baada ya kufuatilia alibaini kuwa kiasi cha Sh milioni 6 ziligawanywa na diwani na mtendaji huyo ambao aliagizwa wakamatwe.
Akitoa maelekzo kwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ukerewe (OCD), alisema diwani na mtendaji huyo wakamatwe kueleza zilipo fedha kiasi cha Sh milioni 6 pamoja na vifaa vya kuezeka ambavyo ni mabati na mbao vilivyonunuliwa kwa Sh milioni 9 na kubanwa warejeshe fedha walizokula.
Alisema nyumba hiyo, ambayo ilijengwa mwaka 2012, haijamazika na kwamba kutokamilika kwake kunakwamisha watumishi kuishi katika nyumba hiyo, jambo ambalo limekuwa likiwakosesha huduma wananchi.
“Unajua huku kwa sababu ni kisiwa watu walikuwa wanajifanyia wanavyotaka, nataka watambue kuwa, kwa sasa tumeamua kuwekea macho Ukerewe na tutashughulika na wabadhirifu na kwa kuanza naomba OCD kamata hawa watoe maelezo ya fedha zetu zilipo na wakirudisha waachie,” alisema.