Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa ametaja mambo matano yanayomkasirisha ambayo yanafanywa na Serikali huku akiionya CCM kuwa ipo siku upinzani utatawala.
Lowassa aliyataja mambo yanayomkera kuwa ni pamoja na kuzuiwa kwa kongamano la kujadili demokrasia ambalo lilipangwa kufanyika jana, sakata la vyeti feki na Serikali kukaa kimya kuhusu mafuriko.
Mengine ni kupaa kwa bei za vyakula na Rais John Magufuli kutohudhuria tukio la kuaga miili ya wanafunzi waliopata ajali ya Karatu, Arusha.
Waziri Mkuu huyo wa zamani, alisema hayo jana wakati akizungumza na wanahabari ofisini kwake Mikocheni wilayani Kinondoni.
Juzi, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano la Demokrasia lililoandaliwa na Chadema, Makongoro Mahanga alitangaza kuwa lingefanyika jana katika Ukumbi wa Arnatouglou, Ilala na wanasiasa wakiwamo viongozi wa CCM na wananchi wa kada mbalimbali wangeshiriki.
Hata hivyo, siku hiyohiyo jioni, CCM ilitoa taarifa ya kukanusha viongozi wake kualikwa katika kongamano hilo.
Sinema iliendelea jana asubuhi wakati Chadema walipotoa taarifa kwa vyombo vya habari wakieleza kuwa uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam umewazuia kutumia ukumbi huo uliopo Mnazi Mmoja.
Akizungumzia zuio hilo, Lowassa alisema amesikitishwa na kitendo hicho alichodai kimefanywa na Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam.
“Tunalaani kitendo hiki kwa lugha inayowezekana, hatua hii ni ya kuminya demokrasia. Nia yetu ilikuwa njema ya kuzungumzia demokrasia.
“Waandaaji wa kongamano hili waliweka picha yangu na ya Kinana (Abdulrahman Kinana-Katibu Mkuu wa CCM) tukionekana tumepeana vichwa lakini tuki- smile (tukitabasamu) jambo ambalo ni very important (muhimu),” alisema Lowassa.
Picha iliyotumika katika tangazo hilo la kuhamasisha kongamano ni ya Kinana na Lowassa wakionekana kuzungumza kwa kunong’ona walipokutana katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Mei 8 katika tukio la kuaga miili ya wanafunzi 32, walimu wawili na dereva waliofariki dunia katika ajali ya basi Mei 6.
Lowassa alisema Tanzania ni moja na watu ni walewale hivyo hakuna tofauti kwa watu wa CCM na Chadema na kwamba kila mmoja kuwa na maoni tofauti hakuna dhambi.
Hata hivyo, Lowassa aliwataka CCM kutambua kuwa ipo siku nchi ya Tanzania itatawaliwa na watu (chama) wengine na siyo wao.
“Kama watashindwa kuondoka wakati wetu, wataondoka wakati wa wajukuu wetu,” alisema.
Alieleza kuwa vyama vya ukombozi duniani vimebaki vichache na katika Afrika anadhani vipo ANC cha Afrika Kusini na CCM, hivyo huo ni ujumbe tosha kwamba ipo siku wataondoka madarakani. Alisema kitendo cha kuwanyanyasa watu kwa sababu wapo upinzani siyo jambo zuri na ni kuminya demokrasia na kushangaa kwa nini halikemewi.
“Waasisi wa Taifa hili wanapaswa kukemea, ndiyo maana tulialika kila mtu katika kongamano lile ili watuambie kwenye demokrasia Chadema mnakosea moja hadi tatu ili tujirekebishe. CCM inakosea hivi na mwisho mnakubaliana cha kufanya,” alisema Lowassa, “Ninalaani kwa nguvu zote kitendo kilichofanywa na Serikali ya Dar es Salaam tusifikishane hapa.”
Kuhusu mafuriko,
Lowassa aliitaja kero nyingine kuwa ni kutoshughulikiwa ipasavyo kwa athari ya mafuriko yanayoyakumba maeneo mbalimbali nchini.
Alieleza masikitiko yake kuwa haoni mkono wa Serikali katika mafuriko hayo ikiwamo kuwapa matumaini wananchi au kiongozi yeyote wa Serikali kuonekana akiwafariji waliofikwa na adha hiyo.
“Nawasifu na kuwapongeza wabunge jana (juzi) waliosimama na kutaka hoja hii ijadiliwe. Nadhani ni muhimu kujadiliwa na kuelezana ili Serikali ijue inafanya nini,” alisema Lowassa.
Bei za vyakula
Mbali na hilo, Lowassa alisema bei za vyakula zimezidi kupanda na wananchi wanapata tabu na kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, mahindi yapo juu kuliko mchele.
“Everything (kila kitu) bei juu. That is problem (hili ni tatizo ) Serikali itaenda kufanya nini katika hili?” alihoji Lowassa.
Alisema binadamu anaishi kwa matumaini, hivyo alitaka kujua wananchi wa vijijini wanapewa matumaini gani kutokana na hali hiyo. Aliiomba Serikali kutangaza na kuchukua hatua za kusaidia upatikanaji wa chakula na mambo mengine ili kuwasaidia Watanzania.
Sakata la vyeti
Kadhalika, Lowassa alizungumzia sakata la watumishi 9,932 wa umma wenye vyeti feki kwamba ubinadamu haujatumika katika kuwafukuza kwa wakati mmoja.
“Siwatetei, lakini wananyimwa mishahara na mafao, wapo waliotumikia kwa miaka 30 au 20. Nakubali kama wamekosea tena sana… Lakini mafao ya mtu, sasa hawa wataenda wapi, mtu ana familia.
“Hata kama walifanya makosa, moyo wa huruma ulihitajika. Sawa amekosa mimi sitetei kosa lao, bali natetea ubinadamu wake, hivi ingenifika mimi leo ungejisikiaje,” alisema.
Alisema anatoa pongezi kwa mambo mengi mazuri yaliyofanywa, lakini katika sakata la vyeti feki, wahusika inabidi wafikiriwe na kwamba shule nyingi zitakosa walimu sanjari na kukosekana kwa wakunga. Alisisitiza kuwa pamoja na nia njema ya Serikali, lakini watumishi hao inabidi waangaliwe kwa sura ya huruma.
Ajali ya Karatu
Akiendelea kuorodhesha kero zake, Lowassa alizungumzia uwakilishi wa Rais Magufuli katika tukio la kuwaaga wanafunzi 32, walimu wawili na dereva wa Shule ya Lucky Vicent ya Arusha waliofariki katika ajali ya basi Karatu.
Alisema yeye binafsi na wakazi wa Arusha walisikitishwa na kitendo cha Rais kutohudhuriatukio hilo lililofanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, Mei 8 badala yake alimtuma Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kumwakilisha.
“Sina mgogoro na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Lakini nasema kuna shughuli hatumwi mtoto, hii haikuwa shughuli ya kutuma mtoto.
“Amiri Jeshi Mkuu, ndiyo mfariji mkuu. Watu wa Arusha walijisikia wanyonge kutomwona Rais katika tukio lile,” alisema Lowassa.
Aliongeza kuwa kitendo cha Rais kutohudhuria kiliwasononesha, kuwahuzunisha na kuwasikitisha wakazi wa Arusha na kwamba anapaswa kwenda kutoa pole kwa wahusika.
Pia alishangwaza na kauli ya Rais Magufuli aliyosema amewasamehe wakazi wa Moshi akiwa katika ziara yake ya kikazi hivi karibuni.
“Unawasamehe kwa kosa gani, kutuunga mkono? Watu milioni sita walisema no (hapana) katika uchaguzi uliopita. Na wana haki, unasema umewasemehe hao,” alihoji Lowassa ambaye mwaka 2015 aligombea urais kwa tiketi ya Chadema na kupata kura milioni 6.03.
“Wewe unawasamehe mimi natafuta nafasi ya kwenda kuwashukuru nanyimwa. Lakini ipo ruksa kwa Rais kuzunguka nchi nzima kwa gari na ndege za Serikali kuwashukuru wapigakura wake, lakini ni dhambi kwa Edward Lowassa,” alihoji.
Lowassa alitumia nafasi hiyo kueleza furaha yake kuhusu ukuaji wa mitandao ya kijamii ambayo alisema inafanya kazi nzuri na akaitaka kuongeza juhudi katika kazi yao na wasikubali kuminywa.
Wakati huohuo, wabunge wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wameitaka Serikali itoe taarifa ya kina kuhusu maafa yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza bungeni jana, Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia alisema maafa hayo yamejitokeza katika maeneo mbalimbali nchini, lakini Serikali imekuwa kimya kuhusiana na suala hilo.
Alisema wabunge wengi wamerudi majimboni mwao kwa ajili ya kuangalia namna ya kuwasaidia wapiga kura wao.
“Pemba zaidi ya nyumba 600 hazifai kabisa zimesombwa na maji na Unguja zaidi ya nyumba 200 na shule zote za Zanzibar zimefungwa miundombinu yake ipo hoi, Tanga maeneo ya Lushoto pia kuna athari kubwa miundombinu ya barabara, shule, taasisi za dini mawasiliano yamekatika,” alisema.
Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo kwa tiketi ya NCCR Mageuzi aliitaja mikoa mingine iliyokumbwa na mafuriko kuwa ni Morogoro, Kagera na Kilimanjaro.
Mbatia ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya majanga alisema Tanzania bado haijajiandaa vya kutosha kukabiliana na masuala hayo, jambo ambalo limekuwa likiwakosesha wananchi taarifa sahihi juu ya majanga mbalimbali yanayoweza kujitokeza na pia kujikinga.
Mbunge wa Malindi, (CUF), Ally Saleh alisema maeneo ya Unguja na Pemba hali ni mbaya na kwamba wanashangaa kwa nini Serikali imekaa kimya kuhusu maafa hayo.
“Jana Serikali imeagizwa ilete taarifa bungeni kuhusu maafa hayo lakini haijaleta, sisi tumefadhaishwa na ukimya huu,” alisema.