Baada ya saa 48 za sintofahamu katika klabu ya Simba, juu ya malalamiko ya Mohamed Dewji kuhusu dili la klabu hiyo na Sports Pesa, jambo lilopelekea kujiuzulu kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Hans Pope (kabla ya kutengua uamuzi wake asubuhi ya leo) – sasa uongozi wa Simba SC kupitia makamu mwenyekiti umetoa taarifa rasmi kwa wapenzi, wanachama na wadau wa soka kiujumla.
Shaffihdauda.co.tz imepokea taarifa hiyo exclusive kutoka kwa Makamu mwenyekiti Godfrey Nyange Kaburu kuhusiana na sakata la Sports Pesa na MO.
Kaburu ameeleza kwamba, uongozi wa klabu jana usiku ulikaa kikao cha pamoja kujadili suala la Sportpesa na MO baada ya taarifa za malalamiko ya Mo kusambaa kwejye mitandao ya kijamii na baada ya hapo kujiuzulu kwa Zakaria Hans Pope.
Uongozi wa Simba uliokaa kikao jana ulifikia maazimio yafutayo:
1. Hanspoppe amerudi kwenye nafasi yake ya ujumbe wa kamati ya utendaji. Hatua ilikuja baada ya kuongea nae na kufikia muafaka wa mambo yaliyopelekea kujiuzulu kwake.
2. Hakuna kiongozi mwingine atakayejiuzulu nafasi yake.
3. Uongozi utakutana na MO muda wowote kuanzia sasa kwa kikao cha pamoja kujadili mapungufu yote yaliyojitokeza na kutengezeza njia sahihi ya kufanikisha malengo tuliyojiwekea
4. Baada ya Kikao na MO kutakuwa na statement ya pamoja itaondoa sintofahamu iliyojitokeza na kutengeneza way forward ili migongano ya aina hii isijirudie.
5. Kwa pamoja Uongozi kwa kushirikiana na wadau wote wa Simba SC waendelee na kampeni ya kushinda mechi mbili zilizo mbele yetu ikiwa pamoja na fainali ya FA Dodoma.
Mwisho Kaburu amesema – “Kwa muda huu ni matumaini yetu kuwa kwa pamoja tutaelekeza dua na nguvu zetu katika mechi 2 zilizobakia. Simba Nguvu Moja.”