Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imepokea kwa masikitiko taarifa ya kuuwawa kwa askari wanane (8) wa Jeshi la Polisi, katika tukio lililotekelezwa na watu wasiofahamika jioni ya Aprili 13, 2017 katika kijiji cha Jaribu Mpakani, Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inalaani vikali mauaji haya ya kikatili ya askari polisi waliokuwa kazini na wasiokuwa na hatia. Aidha, tunaungana na Watanzania wengine kuwapa pole familia za wafiwa na Jeshi la Polisi kwa ujumla.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa matukio ya mauaji ya askari polisi na wananchi wengine maeneo tofauti Mkoani Pwani tangu mwaka 2015 yamekuwa yakiongezeka na kusababisha uvunjifu wa haki za binadamu, hususan haki ya uhai inayolindwa na Katiba ya nchi, na madhara mengine kwa familia za wahanga, kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Haki ya kuishi kama zilivyo haki nyingine, inalindwa kisheria, na pia inalindwa na mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda ambayo Tanzania imeridhia. Hakuna mtu anayepaswa kuporwa haki hii ya msingi kiholela. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) Ibara ya 14, kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria.
Ikumbukwe kwamba askari polisi wanapokuwa kazini wanatekeleza majukumu muhimu ya kulinda raia na mali zao, kwa hiyo usalama wao unategemewa na Watanzania wote. Yeyote yule anayewaua askari polisi siyo tu anataka kuwachonganisha askari polisi na raia, bali pia anawaweka raia hao katika hofu kubwa ya usalama wao na mali zao.
Hivyo basi, kwa mara nyingine, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inashauri kwamba:
1. Katika kuhakikisha kuwa haki ya kuishi ya askari polisi na wananchi wote inalindwa, Jeshi la Polisi na Serikali kwa ujumla wafanye uchunguzi wa kina ili kubaini sababu za mauaji haya kutokea kwa kujirudia Mkoani Pwani, na kuhakikisha wahusika wote wanapatikana na wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria, ili sheria ichukue mkondo wake.
2. Tume inawakumbusha wananchi kuwa vitendo vya ukatili, mauaji, na matendo yote yanayokiuka Sheria yanayofanywa na raia wasio wema ni ukiukwaji wa Sheria, haki za binadamu na misingi ya utawala wa sheira; Hivyo Tume inakemea matendo haya na kutaka yapigwe vita.
3. Aidha, inawataka wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuhakikisha upelelezi wa matukio hayo unakamilika ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa watakaobainika kuhusika na matukio haya.
Imetolewa na:
Bahame Tom Nyanduga
Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Aprili 14, 2017