Hatimaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametekeleza ahadi yake ya kukabiliana na uhaba wa mabweni kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo leo tarehe 15 Aprili, 2017 amefungua mabweni mapya ya wanafunzi wa chuo hicho yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3,840.
Mhe. Rais Magufuli alitoa ahadi ya kujenga mabweni hayo tarehe 02 Juni, 2016 na ujenzi ukaanza tarehe 01 Julai, 2016 ambapo Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kushirikiana na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wamejenga majengo 20 yenye ghorofa 4 kila moja kwa gharama ya Shilingi Bilioni 10, na pia wamejenga uzio wa kuzunguka majengo hayo na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimenunua vitanda, makabati, meza, viti na magodoro kwa ajili ya wanafunzi wote 3,840.
Sherehe za ufunguzi wa majengo hayo zimefanyika ndani ya eneo la mradi na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Mawaziri, Wabunge, Makatibu Wakuu, Wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na viongozi mbalimbali wa Serikali na vyama vya siasa.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof. Rwekaza Mukandala na Rais wa Serikali ya wanafunzi wa chuo hicho (DARUSO) Bw. Erasmi Leon wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutekeleza ahadi yake tena kwa muda mfupi wa chini ya miezi 8, na wamemuhakikishia kuwa Jumuiya ya chuo hicho inamuunga mkono katika jitihada zake za kujenga Tanzania imara chini ya kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu”.
Pamoja na kuelezea furaha yake ya kufanikiwa kwa ujenzi wa mabweni hayo, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza TBA na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa juhudi kubwa zilizofanyika kuharakisha ujenzi huo na kwa gharama nafuu, na ametaka mradi huo uwe mfano wa kuigwa kwa miradi mingine itakayotekelezwa nchini kote.
“Nilipowaambia wataalamu wanipe makadirio ya gharama za ujenzi wa mradi huu waliniambia utagharimu kati ya Shilingi Bilioni 150 hadi 170, nikamuita Mtendaji Mkuu wa TBA Bw. Mwakalinga nikamuambia kuna Bilioni 10 za kujenga mabweni haya.
“Sasa naambiwa kwenye miaka ya 2000 kulijengwa mabweni ya wanafunzi kule Mabibo, mabweni yale yanachukua wanafunzi 4,000 na yaligharimu Shilingi Bilioni 27, sisi hapa tumejenga mabweni mwaka 2017 yanachukua wanafunzi 3,840 na yamegharimu Shilingi Bilioni 10, sasa hapo mtapiga mahesabu wenyewe” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli ameagiza wanafunzi watakaoishi katika mabweni hayo mapya walipie Shilingi 500/= kwa siku badala ya Shilingi 800/= na amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuwapigania wanyonge na masikini kwa kuhakikisha wanapata haki ya elimu ikiwemo mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
Mhe. Rais Magufuli amekubali mwaliko wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wa kwenda kufungua Kampasi ya Mloganzila ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) lakini ameagiza chuo hicho kitakapofunguliwa wanafunzi wote wanasomea masomo ya tiba katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wahamishiwe Mloganzila.
Wakati huo huo, Rais Dkt Magufuli ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU) kuacha kuwachagulia wanafunzi vyuo vya kwenda kusoma na badala yake wawaache wanafunzi wachague wenyewe, na wawapeleke wanafunzi kwenye vyuo watakavyo vichagua.
Wingi wa vyuo katika nchi sio tija, tija ni ubora wa vyuo hivyo. Unaweza ukawa na vyuo vinne vyenye wanafunzi wengi wa kutosha ikawa bora kuliko kuwa na vyuo rundo wambavyo vingine havina wanafunzi, alisema Rais Magufuli.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akilakiwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Profesa Rwekaza Mukandala wakati akiwasili kuzindua majengo mapya ya mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam eneo la Mlimani jijini Dar es salaam. Kiushoto ni Mama Janeth Magufuli na kulia ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Arch. Elius Mwakalinga. Mabweni hayo yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3840, yamejengwa chini ya muda wa mwaka mmoja na yamegharimu shilingi bilioni 10.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongozana na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Profesa Rwekaza Mukandala wakati akiwasili kuzindua majengo mapya ya mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam eneo la Mlimani jijini Dar es salaam.Mabweni hayo yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3840, yamejengwa chini ya muda wa mwaka mmoja na yamegharimu shilingi bilioni 10.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea zawadi ya mchoro toka kwa Rais wa Wanafunzi wakati wa sherehe za kuzindua majengo mapya ya mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam eneo la Mlimani jijini Dar es salaam. . Mabweni hayo yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3840, yamejengwa chini ya muda wa mwaka mmoja na yamegharimu shilingi bilioni 10.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia wakati wa sherehe za kuzindua majengo mapya ya mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam eneo la Mlimani jijini Dar es salaam. Kulia ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Arch. Elius Mwakalinga. Mabweni hayo yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3840, yamejengwa chini ya muda wa mwaka mmoja na yamegharimu shilingi bilioni 10.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipongezwa na na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Profesa Rwekaza Mukandala wakati akielekea kuzindua majengo mapya ya mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam eneo la Mlimani jijini Dar es salaam. Mabweni hayo yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3840, yamejengwa chini ya muda wa mwaka mmoja na yamegharimu shilingi bilioni 10.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisaidiana na viongozi wengine akizindua majengo mapya ya mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam eneo la Mlimani jijini Dar es salaam. Kulia ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Arch. Elius Mwakalinga. Mabweni hayo yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3840, yamejengwa chini ya muda wa mwaka mmoja na yamegharimu shilingi bilioni 10.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipata maelezo toka kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Arch. Elius Mwakalinga wakati akizindua majengo mapya ya mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam eneo la Mlimani jijini Dar es salaam. Mabweni hayo yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3840, yamejengwa chini ya muda wa mwaka mmoja na yamegharimu shilingi bilioni 10.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipongezwa na Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba baada ya kuzindua majengo mapya ya mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam eneo la Mlimani jijini Dar es salaam. Kulia ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Profesa Rwekaza Mukandala Mabweni hayo yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3840, yamejengwa chini ya muda wa mwaka mmoja na yamegharimu shilingi bilioni 10.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akikagua baadhi ya mabweni baada ya kuzindua majengo mapya ya mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam eneo la Mlimani jijini Dar es salaam. Mabweni hayo yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3840, yamejengwa chini ya muda wa mwaka mmoja na yamegharimu shilingi bilioni 10.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia jambo na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Profesa Rwekaza Mukandala (kushoto) na Mkuu wa Idara ya Sanaa za Ubunifu wa Chuo hicho Dkt. Kedmon Mapana baada ya kuzindua majengo mapya ya mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam eneo la Mlimani jijini Dar es salaam. Mabweni hayo yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3840, yamejengwa chini ya muda wa mwaka mmoja na yamegharimu shilingi bilioni 10.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
15 Aprili, 2017