Taarifa ya siku ya nne ya ziara mahsusi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe January Makamba kutembelea mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania yenye lengo la kukagua shughuli za hifadhi ya Mazingira, kusimamia utekelezaji wa sheria za mazingira pamoja na kuangalia namna bora zaidi ya kusaidia serikali za mitaa na mamlaka za wilaya na mikoa ili kuzijengea uwezo mkubwa zaidi wa kusimamia hifadhi ya mazingira pamoja na sheria za mazingira.
Waziri Makamba ameendelea na ziara yake katika mkoa wa Tanga kwa kutembelea na kukagua shughuli za hifadhi ya Mazingira katika wilaya za Muheza na Korogwe ambapo akiwa katika wilaya ya Muheza amepokea taarifa ya mazingira ya wilaya toka kwa Mkuu wa Wilaya hiyo Eng. Mwanasha R. Tumbo.
Mbali na mafanikio yaliyofikiwa na wilaya ya Muheza yaliyoainishwa katika taarifa hiyo Eng. Mwanasha pia aliainisha changamoto kadha wa kadha za uhifadhi wa Mazingira zinazoikabili Wilaya ya Korogwe. Ametanabaisha kuwa kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi wilaya yake inapata mvua mara 1 au 1 na nusu kwa mwaka tofauti na mara 3 kwa mwaka kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Vilevile ameainisha kuwa wilaya imeweka zuio la ukataji miti pamoja na operesheni panda miti ili kurejesha uoto ambao umeathiriwa na shughli za kibinadamu, shughuli ambazo zilichangia kwa kiasi kikubwa mtitiriko mchache wa maji katika maeneo ya wilaya hiyo. Ameeleza pia kuna jitihada za kufukia mashimo yaliyochimbwa na wachimbaji haramu wa madini huku leseni 17 za madini zikifutwa kutokana na wahusika kufanya uchimbaji katika vyanzo vya maji hasa chanzo cha mto Zigi.
Akipokea taarifa hiyo Waziri Makamba amepongeza jitihada kubwa za utunzaji wa Mazingira zinazofanywa na Wilaya ya Muheza ambapo ameeleza kuwa serikali inalenga kuweka katika bajeti zake fungu la mazingira kila mwaka kwa halmashauri nchi nzima ambazo zitasaidia katika kusimamia miradi ya hifadhi ya mazingira lakini pia ameeleza kuwa mfuko wa hifadhi ya mazingira ulioanzishwa wenye jukumu la kutafuta fedha kutoka vyanzo nje ya bajeti utasaidia kupata fedha za kusimamia miradi mbalimbali ya mazingira itakayoanzishwa.
Akiwa njiani kuelekea katika hifadhi ya mazingira ya asili Waziri Makamba amefika katika kijiji cha Kisiwani eneo la Fanusi kuona na kukagua mradi wa ufugaji Vipepeo unaofanywa na unaonufaisha wakazi wa kijiji hicho. Baada ya kukagua na kujionea jitihada kubwa za uhifadhi mazingira zinazofanywa na wanakijiji hao waziri Makamba ameweka wazi kuwa Kijiji hicho ni mfano wa kuigwa katika maana nzima kunufaika na uchumi wa kijani ambao hauathiri hifadhi ya mazingira lakini pia ni mfano wa moja kwa moja wa manufaa ya hifadhi ya mazingira kwa jamii. Akiwa katika mradi huo baada ya kukagua na kupokea taarifa ya mradi Waziri Makamba ameahidi kushughulikia upatikanaji wa vibali vinavyohitajika ili kuwezesha uuzwaji wa vipepeo lakni pia ameahidi vibali husika vikishapatikana atajenga vibanda 10 vya kuzalishia vipepeo katika eneno hilo ikiwa kama ishara ya kutambua na kupongeza jitihada kubwa za uhifadhi mazingira zinazofanywa na mradi huo.
Waziri Makamba pia amepata wasaa wa kutembelea na kukagua hifadhi ya mazingira ya asili Amani (Amani Nature Forest Reserve) ambayo mbali na kuwa moja kati ya hifadhi asili yenye vyanzo vingi vya maji pia inasifika kwa kuhifadhi gesi ukaa, kuwa na viumbe hai ndwele/adimu wanaopatikana katika hifadhi ya Amani pekee Dunia nzima kama vile ua la dungulushi (African Violet) huku pia ikiwa ni sehemu nyeti kwa mafunzo na tafiti za misitu ya asili ya tropiki ambayo ni michache sana.
Akisoma taarifa ya mazingira ya hifadhi hiyo, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya misitu ya asili ya Amani, Bi Mwanaidi Kijazi ameeleza changamoto mbalimbali zinazoikabili hifadhi hiyo zikiwemo uanzishwaji wa moto wakati wa kuandaa mashamba,ukataji wa miti hasa mivule kwaajili ya mbao, uchimbaji madini katika vyanzo vya mito hususani chanzo cha mto Zigi pamoja na upatikanaji kwa urahisi wa leseni za uchimbaji na utafutaji madini kwa wachimbaji wadogo (Primary mining license) jambo linalowapelekea kuchimba bila ya kufuata kanuni na sheria za utunzaji na uhifadhi mazingira.
Kabla ya kutembelea na kukagua maeneo ya hifadhi yaliyoathiriwa na wavamizi wanaofanya shughuli za kibinadamu Waziri Makamba amepanda mti ikiwa ni kielezo cha kuunga mkono operesheni kupanda miti katika hifadhi hiyo. Baada ya zoezi la upandaji miti Waziri Makamba amefika na kujionea uharibifu mkubwa katika bonde la Zigi ambalo ni chanzo cha mto Zigi unaofanywa na wavamizi wanaojishugulisha na uchimbaji haramu wa dhahabu kinyume na taratibu.
Baada ya kukagua maeneo yaliyoathirika Waziri Makamba alipokea taarifa ya usimamizi wa hifadhi ya mazingira kabla ya kupata wasaa wa kuzungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi walijitokeza kumsikiliza. Katika taarifa hiyo Waziri Makamba ameombwa kuhakikisha mipango thabiti na taratibu za kudhibiti shughuli za uchimbaji haramu wa madini zinawekwa ikiwemo kuweka utaratibu wa kuwataka wenye vibali vya uchimbaji na utafutaji madini (primary mining license) kufanya tathmini ya uharibifu wa mazingira kabla ya kupewa kibali na kuanza zoezi la kuchimba au kutafuta madini.
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara Waziri Makamba kwanza alipongeza jitihada zinazofanyika zenye lengo la kuokoa mazingira yanayovamiwa na wavamizi ikiwemo kufuta leseni 17 za uchimbaji wa madini lakini pia jitihada za kufukia mashimo na kupanda miti inayohimili maeneo ya majimaji katika maeneo yaliyoathirika na uchimbaji (jitihada aliyoiunga mkono kwa vitendo kwa kupanda mti) ili kurudisha hali ya uoto wa asili, vilevile Waziri Makamba ameeleza serikali itashughulikia tatizo la ukosefu wa maji kwa maeneo jirani hifadhi na italeta mradi mkubwa wa maji Muheza lakini zaidi amewataka kutunza vyanzo vya maji kwani ni vyanzo hivyohivyo vitatumika katika miradi itakayoanzishwa ili kusambaza maji kwao (wananchi)
Akizungumzia tatizo la uvamizi na uchimbaji madini katika vyanzo vya mito hasa katika chanzo cha mto Zigi Waziri Makamba alisema, ”Tumefika hapa kuona, kukataza na kuzuia shughuli zote za uharibifu wa mazingira, shughuli ambazo zinahatarisha uwepo wa hifadhi yetu, na hii inajumuisha shughuli za uchimbaji haramu wa madini katika vyanzo vya maji. Yeyote atakayekamatwa atafikishwa mahakamani, atafungwa na ninawahakikishia kuwa hakutakuwa na mzaha katika hili, serikali haitokubali mashimo mengine yatokee tena kwasababu ya uchimbaji haramu”.
Waziri Makamba ametoa pongezi kwa mkuu wa wilaya ya Muheza Eng Mwanasha Tumbo, kamati ya ulinzi na usalama, wananchi watunza mazingira pamoja wanamazingira wa hifadhi ya Amani kwa kazi kubwa kuhakikisha sio tu wanapambana na kuwadhibiti waharibifu bali pia juhudi za upandaji miti katika mashimo yaliyoachwa na wachimbaji haramu ili kurejesha sehemu zilizoathiriwa katika hali yake ya awali huku pia akipongeza jitihada kubwa zilizofanywa kwa ushirikiano na ofisi ya bonde la Pangani pamoja na UNDP zinazolenga kuanzisha kwa kituo cha polisi ndani ya eneo la hifadhi ili kushughulukia na kupambana kwa ukaribu na waharibifu wa mazingira ambapo ameahidi kushughulikia kwa haraka ombi la kujenga makazi watakayoishi polisi wa kituo hicho pamoja na upatikanaji bajeti ya shughuli za utunzaji mazingira.
Baada ya kuhitimisha shughuli katika wilaya ya Muheza Waziri Makamba amefika katika wilaya ya Korogwe ambapo kabla ya kupokea taarifa ya mazingira ya Wilaya iliyowasilishwa na Mkuu wa wilaya ya Korogwe Gabriel Robert iliyoainisha changamoto mbalimbali za kimazingira Waziri Makamba alishiriki katika zoezi la upandaji miti katika eneo la kata ya Hale, Kijiji cha Mwakinyumbi-Miembeni karibu na mto Pangani. Taarifa ya wilaya iliyowasilishwa na imeonesha changamoto mballimbali za uharibifu wa vyanzo vya maji, uchomaji moto mashamba wakati wa kuandaa kwaajili ya kilimo moto ambao husambaa na kuchoma maeneo ya jirani, vilevile imeainsha uvunaji holela wa mazao ya misitu usiofuata na kuzingatia taratibu.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa kata ya Hale waliojitokeza kumsikiliza Waziri Makamba amewaasa wananchi wa Hale kushiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi wa mazingira ni dhahiri kuwa uendelevu wa maisha kwa kiasi kikubwa unategemea uhifadhi wa mazingira.
“Dunia hii, ardhi na rasilimali zilizopo hapa Hale sisi hatukuzirithi kwa vizazi vilivyopita, sisi tumeiazima kwa vizazi vijavyo na tukisema tumeazima tunapata mtazamo kwamba tunatakiwa tuzirejeshe zikiwa katika hali ileile au pengine nzuri zaidi ili wanaokuja wakute ipo katika hali wanayoweza kutengeneza maisha”. Alisisitiza Waziri Makamba
Waziri Makamba anatarajiwa kukamilisha ziara yake katika mkoa wa Tanga hivi leo na kuendelea katika mkoa wa Kilimanjaro.