Inawezekana unahitaji kujua sababu za kiufundi kwa nini Yanga wameshindwa kupata ushindi kwenye mechi yao ya kimataifa dhidi ya Zanaco wakiwa nyumbani kwenye uwanja wa taifa na kujikuta wakilazimishwa sare ya kufungana goli 1-1 baada ya dakika 90.
Kocha msaidizi wa Yanga Juma Mwambusi amesema, sababu kubwa ya timu yao kutofanya vizuri kwenye mchezo huo ni uchovu walionao wachezaji unaotokana na kucheza mfululizo huku majeruhi pia wakichangia kudhoofisha kikosi chao.
“Kinachowasumbua wachezaji wangu ni uchovu na kwa sababu tumefululiza sana kucheza, ratiba katika kipindi hiki imekuwa ngumu sana kwetu, wachezaji hawana miili ya chuma. Tumejaribu kuwarejesha mapema wachezaji ambao walikuwa majeruhi lakini hawajaweza kuwa msaada mkubwa kwenye timu kutokana na hali yao,” – Juma Mwambusi.
“Kwa hiyo tukipata muda wa kupumzika tutaweza kufanya vizuri kwenye mechi ya marudiano.”
“Niwapongeze Zanaco kwa kuweza kurudisha goli katika kipindi cha pili baada ya makosa ya safu yetu ya ulinzi tukaruhusu hilo goli. Lakini mpira haujaisha bado tunaweza kwenda kwao Zambia na tukapata ushindi,malengo yetu na matarajio ni kupata ushindi kikubwa tumewajua Zanaco kwa sababu kabla ya mchezo wetu dhidi yao tulikuwa hatuwafahamu.”