SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 1 Machi 2017

T media news

Makonda ameanza ukarabati wa viwanja vya Ndondo Cup

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Mh. Paul Makonda jana alitembelea uwanja wa Boko Veteran ikiwa ni sehemu ya kujionea namna ya kuboresha baadhi ya viwanja ambavyo vitatumiwa katika michuano ya Ndondo Cup kama alivyoahidi msimu uliopita.

“Hapa tumefika ikiwa ni sehemu ya kuangalia shauku yetu kubwa ni kuona namna gani tunaweza kupata uwanja mzuri kwa sababu tuna vitu viwili, tuwe na uwanja wa nyasi bandia au uwanja wa nyasi halisi za kupandwa,” amesema Makonda alipotembelea uwanja wa Boko Veteran.

“Kwahiyo tumekuja hapa kuona sehemu ambayo ni maeneo yaliyotengenezwa kwa nyasi halisi, lakini uwanja tunaotarajia kuanza nao ni ule wa Bandari kwa sababu unatumika mara nyingi na wananchi wanaokaa maeneo ya jirani na pale.”

“Tunashirikiana na wenzetu wa ubalozi wa China ambao tulimuomba balozi wa China ambaye hayupo hapa lakini tumekuja na wasaidizi wake kwa ajili ya kuona lakini ndani ya wiki hii tutakuwa tumefanya maamuzi kama tutajenga uwanja wa nyasi bandia au nyasi halisi ili msimu wa Ndondo Cup utakapoanza angalau uwanja mmoja uwe umeshakamilika.”

Msimu uliopita wa michuano ya Sports Extra Ndondo Cup, serikali ya mkoa wa Dar es Salaam kupitia kwa mkuu wake wa mkoa Mh. Paul Makonda iliahidi kuboresha miundombinu kwa kutengeneza mahali pa kuchezea soka (pitch) baada ya kufika kwenye viwanja ambavyo vilikuwa vinatumiwa na vijana wakati wa mashindano hayo na kutoridhishwa na hali ya viwanja.