Simon Msuva ni mchezaji wa Yanga ambaye kwa sasa yupo kwenye kiwango bora kiuchezaji, aliweza kuifungia timu yake bao dhidi ya Zanaco kwenye mechi ya klabu bingwa Afrika March 11, 2017 kwenye uwanja wa taifa lakini goli hilo halikudumu kwa dakika 90 kutokana na Zanaco kusawazisha dakika ya 77 ya mchezo.
Msuva anaamini Yanga inaweza kufanya vizuri hata ikiwa ugenini kama watatumia vizuri muda walionao katika mazoezi na kurekebisha makosa ambayo benchi lao la ufundi tayari limesha yabaini.
“Tumepata sare kwenye uwanja wa nyumbani walimu watakuwa wameona makosa na watatuambia ni vitu gani vya kufanyia marekebisho, bado tuna muda wa kufanya mazoezi na kujipanga. Tunaweza kufanya vizuri hata huko kwao kwa sababu mpira hautabiliki.”
Msuva ameshafunga magoli mawili kwenye michuano ya Afrika msimu huu katika mechi tatu ambazo amecheza.