SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 26 Aprili 2017

T media news

Miaka 53 ya Muungano: Hoja ya Serikali tatu iko pale pale

WAKATI Muungano wa Tanganyka na Zanzibar ukifikisha miaka 53 tangu ulipoanzishwa Aprili 26 mwaka 1964, bado hoja na madai ya kuwepo kwa Muungano wa Serikali tatu imeendelea kuvitikisa viunga vya siasa na upepo wake kuvuma ukipenya katika masikio ya wananachi wa Bara na Visiwani.

Pengine kuundwa kwake Muungano huu huko nyuma kama kungekosekana nguvu za kisiasa za vyama vya TANU na ASP kungekuwa na mbinde ya suala hilo kufikiwa muafaka na mapatano kutokana na ugumu wake kulingana na mazingira tata yaliokuwepo katika pande mbili za Muungano.

Wapo wanaosema kwamba historia ya nchi mbili hizi, mwingiliano wa watu wake, mila, desturi, tamaduni, makabila na hata harakati za uendeshaji biashara, kumeyasukuma mno mawazo ya kuwepo kwa Muungano hadi kupatikana kwa wepesi na kuziunganisha nchi hizo.

Wengine wanaeleza kuwa uhusiano wa tangu na tangu, zama na zama ikiwemo miaka kwa miaka kati ya Jumuiya za TAA ya Tanganyika na African Association ya Zanzibar , baadaye kuanzishwa TANU na ASP, tangu la uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi ya Zanzibar ni katika jumla ya mambo yaliyohimiza na kutia chachu ilikuwa na taswishi ya kuundwa kwa Muungano.

Pamoja na kuwemo kwa mambo hayo pia urafiki, mahusiano ya kiasili, kijamii na udugu wa damu wa vyama na Jumuiya za TAA, hadi TANU /ASP , licha ya kuelezwa ndiko kutia mshawasha, wapo wanaosema hata shabaha na malengo ya jumuiya na vyama hivyo yalifanana.

Upande mwingine unaeleza ikiwemo na maandiko ya baadhi ya vitabu vya kisiasa, vinaeleza kuwa viongozi na vyama vya ukombozi barani Afrika wakati wakiwa katika harakati za kupigania uhuru, mikutano na vikao vya washirika wa umoja wa umajumui yaani Pan Africanism, maazimio mengi yalikuwa yamejiegemeza na kuazimia kuwa baada ya kujikomboa, Afrika iwe na dola moja.

Hata hivyo, yote hayo yanapotazamwa kwa macho tofauti, pia inaelezwa vyama pinzani vya United Tanganyika Party (UTP) na African National Congress (ANC) kwa upande wa Tanganyika pamoja na kuwa dhaifu kisiasa, vilipinga jambo hilo huku ZNP na ZPPP vya Zanzibar navyo havikuunga mkono wazo la Muungano , zaidi ikitajwa vilikuwa zimezingwa na hamaki iliyotokana na makovu ya kupinduliwa na ASP .

Lipo kundi linalodai wananchi wa pande mbili za Muungano hawakuulizwa, hakukuitishwa kura ya maoni ili maamuzi ya hapana au ndiyo yaweze kupatikana kidemokrasia.

Badala yake vigogo wawili yaani Mwalimu Julius Nyerere na sheikh Abeid Karume waliafikiana na kuanza kuandikwa mkataba wa muungano uliokuwa na mambo 11 tu ambayo ilitakiwa yapitiwe tena baada ya miaka kumi.

Wengine wanapinga dai hilo na kusema serikali ya ASP iliwauliza wananchi wa Zanzibar katika mikutano ya hadhara huku akisikika hayati Mzee Karume akiwauliza Wazanzibari kwa kauli mbiu yake ya"je wananchi mko tayari kwa Union?”

Inaelezwa kuwa hiyo ilikuwa ni kura ya maoni tosha na walioafiki ni wananchi kupitia chama tawala cha wakati huo ASP kwasabahu isingetarajiwa wananchi ambao ni wana ZNP /ZPPP wasiafiki jambo hilo.

Azimio la kuundwa Muungano linaelezwa lilifanyika kwa kuzingatia misingi, ridhaa na ruhusa ya wananchi wenyewe.

Baadhi ya watu wanamtaja na kuona Mzee Karume alikuwa na kipaji cha ajabu na kiongozi anayetazama mbali kila wakati. Uamuzi wa chama chake akiwa Rais wa ASP kukubali rai ya kuungana ilikuwa ni njia sahihi kwa usalama wa maisha na utawala wake .

Kwakuwa alitambua yeye na chama chake walichukua madaraka kwa njia ya Mapinduzi , angeendelea kuamini na kukubali abaki kuongoza serikali ya Zanzibar bila ya kuwa na nguvu za umoja na kuunda nchi moja yenye Jamhuri na dola kamili, asingetamba ila naye angepinduliwa kama alivyopindua.

Kuona kwake huko mbali Mzee Karume katika kujua kwake Zanzibar ina ardhi ndogo, rasilimali na maliasili kidogo huku ikikabiliwa na idadi haba ya watu , aliiona Tanganyika ikiwa ni nchi kubwa yenye utajiri , ardhi na maeneo ya kilimo.

Baada ya Mapinduzi mwaka 1964 Serikali ya ASP mara moja kwa kutumia matamko ya Rais ilipiga marufuku kisheria mfumo wa vyama vingi na kuanzishwa mfumo wa chama kimoja kwa kile kilichoelezwa vyama vingi ni mfumo wa fitna unaozaa mgawanyiko katika jamii .

Mwaka 1965 Tanganyika nayo kupitia bunge ilifuta kisheria mfumo wa vyama vingi na kuongozwa na chama kimoja kwa miaka 19 hadi pale uliporejeshwa tena kisheria mfumo huo mwaka 1992 chini ya kivuli cha serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ingawa kwa miaka mingi hakukuwa na jukwaa lililofanya sauti za upande mwingine zisikike katika kukosoa au kushauri, kwa mara ya kwanza hoja ya utata na kutaka Muungano wa serikali tatu ikaibuka hadi kutinga mezani kwa Rais na Mwenyekiti wa CCM , Mwalimu Julius Nyerere.

Hoja hiyo iliibuliwa na mtu mzito. Msomi, gwiji wa kujenga hoja na hodari wa kupambanua mambo , aliyekuwa Rais wa ASP ambaye wakati alijaribu kumkata" jongoo kwa meno yake " yeye bado ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Makamo wa kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hayati Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi.

Jumbe atakumbukwa kwa mengi ila kimbunga na masahibu mazito yamekatisha mustakabali wake kisiasa . Mzee huyo akaondoshwa madarakani akiwa na Waziri Kiongozi wake Ramadhan Haji Faki.

Ndoto na kiu ya mzee Jumbe ikazimwa, joto likaongezeka na vuguvugu la madai ya kuwepo kwa muungano wa serikali tatu yakabaki pale pale.

Hata hivyo, Mze Jumbe alitoswa na kundi la wazanzibari wenziwe akapotea mkondoni wakiongozwa na Mwanasiasa Mkongwe Visiwani Maalim Seif Sharif Hamad.

Joto la dai hilo likafanikiwa kuzimwa na Rais Julius Nyerere ambaye aliwahi kutamka hadharani mara kadhaa katika uhai wake kwamba mtu yeyote kuzungumzia kuvunja Muungano ni sawa na kutenda dhambi ya uhaini.

Madai ya chini kwa chini yakaendelea kuwepo, wapo walioonekana kushiriki madai hayo kwa tamaa ya kupata madaraka na vyeo huku baaadhi yao wakishirikiana na wapinzani asili wa Muungano waliohamia na kuishi ughaibuni .

Katika hali isiotarajiwa chini ya utawala wa Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa pili wa Rais Mzee John Malecela, hoja ya serikali tatu ikafikishwa bungeni, wabunge 55 wakaandika majina yao na kusainii wakitaka uwepo muundo wa serikali tatu .

Kundi la wabunge hao likaoongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Lupa Njelu Kasaka. Bunge likakatika pande mbili.Wapo waliotaka ubaki Muungano wa serikali mbili kwasababu kuwa na serikali tatu ni kuuvunja muungano wenyewe.

Kama kawaida yao wabunge kutoka Zanzibar hawakuandika majina yao. Wenzao wa Bara walipowauliza mbona hawaandiki majina kuwaunga mkono , wakajibu wao wana yao iitwayo SMZ hivyo wakatakiwa wale wa Bara waendelee kudai mpaka nao wapate serikali yao.

Mwalimu Nyrerere akautazama mwenendo wa wabunge 55, akaisadisi misimamo yao , kusililiza masuala na madai yao kikaitishwa kikao cha NEC jijini Dar es salaam, wabunge nao wakaalikwa.

Mwalimu Nyerere akahudhuria kama mgeni mwalikwa ambapo aliingia na hoja yenye maneno mawili tu .

Neno la kwanza akataka wabunge wanaopigania serikali mbili wasimame upande mmoja wakiandika na kusaini majina yao, wale wa Muungano wa serikali tatu pia nao wafanye hivyo huku wakitakiwa kuweka kadi ya CCM mezani.

Madai ya Mwalimu Nyerere yakajiegemeza katika maeneo mawili makuu. Akaeleza muundo wa serikali mbili si sera ya CCM. Anayeunga mkono msimamo wa sera ya chama atabaki kuwa mwanachama mwaminifu na yule anayetaka serikali tatu aipinge CCM akiwa nje ya chama hicho.

Eneo la pili ni la shutuma na lawama kwa viongozi wakuu wawili muhimu serikalini na kisiasa. Akalaumiwa Waziri Mkuu Malecela akiwa msimamizi mkuu wa shughuli za serilali bungeni kwanini aliruhusu mjadala huo, pia akalaumiwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM hayati Horace Kolimba kwa kushindwa kusimamia sera na msimamo wa chama.

Wote wawili wakalazimika kuwajibika na kuachia nafasi zao hivyo dai hilo la muundo wa serilali tatu likazimwa na mwalimu Nyerere kwa nguvu ya hoja hiyo na kuwa tamati ya mjadala huo.

Mwanasiasa wa upinzani katika chama cha Democratic Party (DP)hayati Mchungaji Christopher Mtikila atakumbukwa kwa kuonyesha msimamo wa kupigania Tanganyika irejee na kuwa Taifa huru huku akikataa kusajili chama chake kwa udhamini wa wanachama toka Unguja na Pemba kama Sheria No 5 ya mwaka 1992 isemavyo.

Msimamo wake huo ukamvuruga. Akachelewa kupata usajili wa chama hicho hadi pale alipobwaga manyanga na kupata uwakilishi toka upande wa pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hoja hiyo nayo ikafifishwa na kutiwa kapuni kama zile za jumbe na ile ya Kasaka na wabunge 55 waliotaka kulifufua Taifa la Tanganyika wakati mkataba wa Muungano ukisema kutakuwa na muundo wa serikali mbili.

Mjadala wa serikali tatu ukaongozwa na Tume ya marekebisho ya katiba iliyoongozwa na jaji mstaafu Joseph Warioba wakiwemo na wanasiasa wakongwe Waziri Mkuu wa zamani Salim Ahmed Salim, aliyekuwa msaidizi wa Nyerere Joseph Butiku, wanasheria Dk. Sengondo Mvungi, Awadhi Ali Said, Ali Saleh wakiwemo na wanasiasa vijana Simai Mohamed Said na Katibu Mwenezi wa CCM Polepole wakati wa enzi ya utawala wa Rais mstaafu Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.

Pamoja na Tume ya Warioba na baadhi ya makamishna wake kuonekana wakiwa na msimamo wa kuupigia debe muundo serikali tatu, mpango huo ukapingwa vikali na wana CCM wengi huku mjadala huo ukihitimishwa na Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete wakati akilihutubia Bunge Maalum la Katiba na kuwa chimbuko la kuzaliwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (ukawa) mwaka 2015.

Hata hivyo, wanachama wawili wa CCM kutoka Zanzibar akiwemo aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria katika serikali ya Muungano Hassan Nassor Moyo na mwenzake aliyekuwa Waziri katika serikali ya Rais Amani Karume, Mansoor Yussuf Himid kwa kuonyesha kutaka uwepo Muungano wa serikali tatu
ikasababisha kufukuzwa uanachana ndani ya CCM kabla ya kuungana na CUF na kuanza kupigania mamlaka kamili ya Zanzibar katika mfumo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Miaka 53 ya Muungano wakati ikiadhimishwa hoja ya muundo wa serikali tatu bado iko hai, mbichi ingawa hakuna anayeweza kutamka madai hayo akiwa ndani ya CCM huku akibaki salama pasi na kutoswa .