IMEFAHAMIKA kuwa kuhojiwa tena kwa Askofu Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la jijini Dar es Salaam jana kulitokana na tuhuma zilizomfanya ahojiwe awali na Polisi kuhusiana na dawa za kulevya.
Jana, taarifa zilisambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kuelezea kuwa mchungaji huyo anashikiliwa tena na polisi na kwamba, alikwenda kupekuliwa nyumbani kwake, eneo la Salasala jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, akizungumza na Nipashe kuhusiana na tarifa hizo, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polis, Simon Sirro, alisema ni kweli wamemhoji Gwajima kuhusiana na tuhuma zilezile zilizomfanya ahojiwe nao awali, lakini hawamshikilii.
Gwajima aliwahi kuhojiwa na polisi baada ya kutajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda katika orodha ya watu wanaohusishwa na dawa za kulevya.
“Gwajima aliripoti leo (jana) hapa kituoni kwa kosa lile lile la awali la dawa za kulevya ambalo alipewa dhamana… alikuja na kuondoka nyumbani, hatumshikilii,” alisema.
Awali, baada ya kusambaa kwa taarifa za kushikiliwa kwa Gwajima,
msaidizi wake wa karibu, Maxmillian Machumu alikiri kiongozi huyo kuwa polisi lakini akiongeza kuwa hawajui ni kwa kosa gani.
“Hatuelewi mashtaka yanayomkabili polisi hawajayaweka wazi, wamemkamata baada ya leo (jana) asubuhi kwenda kituo cha Polisi Kati, wamemchukua na kwenda naye nyumbani kwake na kumpekuwa mida ya saa 3:00 asubuhi,” alisema.
Februari 8, mwaka huu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alitangaza hadharani majina 65 ya watuhumiwa wa dawa za kulevya akiwamo Askofu Gwajima na pia baadhi ya wafanyabiashara, wanasiasa na wasanii.