SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 10 Machi 2017

T media news

Bulembo atangaza kuachia ngazi jumuiya ya wazazi Ccm

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Bulembo, amesema hatagombea tena nafasi hiyo wakati wa uchaguzi ujao wa jumuiya hiyo.

Chama Cha Mapinduzi na Jumuiya zake zinatarajiwa kufanya chaguzi zake mbalimbali mwaka huu.

Bulembo, ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, aliyasema hayo jana mjini hapa, katika mkutano wa dharura wa jumuiya hiyo.

Alisema kwamba, ameamua kutogombea nafasi hiyo ili wengine waweze kuongoza jumuiya hiyo.

“Mimi siyo king’ang’anizi wa madaraka na ndiyo maana nafasi nyingi za uongozi nimekuwa nikizishikilia na kuziachia ili wengine nao wapate fursa ya kuongoza.

“Kwa hiyo, nasema mwaka huu sitagombea, kwani ndio mwaka wa uchaguzi. Naomba msiniulize ni kwanini sigombei.

“Hoja isije kuwa ni ubunge wangu, bali hiyo ni kawaida yangu na historia yangu inaonyesha nimekuwa diwani kwa miaka 15 na nilivyosema naondoka, watu wakaanza kuhoji kwanini ninafanya hivyo.

“Wakati mwingine unatakiwa kuwapa fursa na watu wengine kuongoza na ndiyo maana niliwahi pia kuachia madaraka nilipokuwa kiongozi wa Chama cha Soka Tanzania wakati ule kikiitwa FAT.

“Ila ninachoweza kusema ni kwamba, ninaondoka ndani ya jumuiya yetu na kuiacha ikiwa imara na wala sijawahi kuomba fedha CCM kwa ajili ya kufanya vikao,” alisema Bulembo.

Akizungumzia uchaguzi katika chama hicho, aliwataka wagombea kujipima kama kweli wanafaa kutokana na utendaji kazi wao.

“Kama ulifanya vizuri ndani ya mkoa, utachaguliwa, kama ulifanya vibaya, utakaa pembeni kwa sababu hutachaguliwa.

“Kwa hiyo, msiokuwa na sifa, msiende kuwafanyia figisufigisu watu wanapokwenda kugombea nafasi zenu,” alisema.