Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amesema mtu aliyemtishia kwa bastola aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye si askari wa Jeshi la Polisi, lakini ameshapatikana na atashughulikiwa kwa mujibu wa utaratibu wa ulinzi na usalama.
Mwigulu alisema hayo baada ya kufungua mkutano wa kazi wa mwaka wa maofisa waandamizi wa polisi, makamanda wa mikoa na wakuu wa vikosi wa Jeshi la Polisi ambao unafanyika mjini hapa.
“Ameshapatikana (aliyemtishia Nape) na atashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu za ulinzi na usalama ambazo zimekuwa zikifanyika ndani, lakini hazitangazwi,”alisema.
Hata hivyo, Mwigulu alikataa kuelezea kwa undani kuhusu mtu huyo kwa kubainisha anatoka taasisi gani wala jina la mtuhumiwa kwa madai kuwa ni kwa sababu ya usalama wake.
Baadhi ya taasisi za ulinzi na usalama nchini ni Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Usalama wa Taifa na Takukuru.
Mtu huyo alifanya kitendo hicho wakati Nape, ambaye alikuwa Waziri wa Habari, alipokuwa anaelekea Hoteli ya Protea alikopanga kuzungumza na waandishi wa habari baada ya mbunge huyo wa Mtama kuachwa katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri.
Mtu huyo alikuwa pamoja na wenzake wawili ambao kwa pamoja walikuwa wakimlazimisha arudi kwenye gari lake na kuondoka, lakini Nape alibisha na ndipo mtu huyo aliporudi nyuma, kuchomoa bastola kutoka kiunoni na kisha kumtishia kabla ya kutulizwa na mwenzake.
Watu hao walitoweka eneo hilo muda mfupi baadaye.
Siku moja baada ya tukio hilo Mwigulu alimwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi, Ernest Mangu kumtafuta mtu huyo.
Mwigulu aliandika katika ukurasa wake wa twitter akisema:
“Mh Nape sio jambazi, hana record za uhalifu. Kitendo cha kutolewa bastola si cha Kitanzania na si cha kiaskari. Nimemuagiza IGP achukue hatua.”
Tukio hilo lilitokea siku chache baada ya RC Paul Makonda kuvamia kituo cha televisheni cha kampuni ya Clouds Media, akiwa na askari wenye silaha za moto na kulazimisha arekodiwe mahojiano baina ya watangazaji wa kipindi cha Shirika la Wambeya Duniani (Shilawadu) na mwanamke anayedai kuzaa na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, ambaye ameibukia kuwa mpinzani wa kiongozi huyo.
Hadi sasa, Jeshi la Polisi halijaeleza kuhusu askari hao waliojumuika kufanikisha uvamizi huo.