SHIRIKA la Mpango la Chakula Duniani (WFP) limebadili mfumo wa kuwahudumia wakimbizi na sasa litakuwa linatoa fedha taslimu kwa kila mwanakaya kwa mwezi badala ya kuwapatia chakula.
Jana baadhi ya wakimbizi wanaoishi katika Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu walianza kupokea fedha taslimu kutoka WFP katika hatua za awali za kubadilisha mfumo wa sasa wa kuwapatia chakula kila mwezi.
Taarifa iliyotolewa jana na WFP ilifafanua kuwa wakimbizi 10,000 sasa watapokea fedha taslimu kama sehemu ya mradi wa majaribio wa miezi mitatu. Mradi huu unafadhiliwa na Canada ambayo imetoa Dola za Marekani 385,000 (Sh milioni 808.5) kwa WFP.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, WFP itatoa Sh 10,000 mara mbili kwa mwezi kwa kila mwanakaya wa kaya iliyo katika mradi wa majaribio. Fedha itatumwa kwa mlengwa kupitia mtandao wa simu.
“Katika kipindi chote cha mradi, wakimbizi wataendelea kupata mgawo wa mafuta ya kula yaliyoongezewa virutubisho na mchanganyiko maalumu wa uji wakati ambapo badala ya mahindi, kunde na chumvi wanufaika watapewa fedha taslimu,” ilisema taarifa hiyo.
Utoaji wa fedha taslimu unawapa wakimbizi uhuru wa kuchagua chakula gani cha kununua na wakati huohuo kuingiza fedha katika uchumi wa ndani. Soko la Pamoja la Nyarugusu, lililofunguliwa mwaka huu, ni eneo huru kati ya kambi na jamii ya wenyeji, ambako wafanyabiashara wanapata nafasi ya kuwauzia wakimbizi bidhaa zao.
“Canada inafurahi kusaidia shughuli za WFP za kuhudumia wakimbizi nchini Tanzania,” alisema Balozi wa Canada nchini, Ian Myles na kuongeza kuwa “Kuunganisha msaada wa chakula na fedha taslimu kunawapa wanawake na wanaume uhuru zaidi katika kukidhi mahitaji yao na kunaweza kuwa na matokeo mazuri kwa jamii ya wenyeji.”
Zaidi ya wakimbizi robo milioni wamepata hifadhi nchini Tanzania katika kambi tatu magharibi mwa nchi. Wakimbizi nchini Tanzania hususan kutoka katika nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wanategemea zaidi msaada wa WFP kama chanzo chao kikuu cha chakula. WFP inahudumia zaidi ya watu milioni 80n katika nchi 80 duniani kila mwaka.