Utata umeibuka juu ya kukamatwa kwa msanii wa filamu nchini Steven Mengele a.k.a Steve Nyerere, mara baada ya kuwepo kwa taarifa hizo ambazo zimetolewa ufafanuzi na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro.
Akizungumza jana na wanahabari, Kamishna Sirro alisema yeye hajamuita Steve Nyerere lakini huenda akawa ameitwa na maafisa wake wa upelelezi kwa ajili ya mahojiano, jambo ambalo ni sahihi.
Sirro alisema kuna kikosi maalum alichokipa kazi hiyo na endapo msanii huyo anahojiwa ataweza kuachiwa kama kikosi hicho kitajiridhisha kuwa anastahili dhamana, lakini kama kitaona bado kinamuhitaji, kitaendelea kumshikilia.
Msanii huyo ameingia kwenye 'headline' hasa mitandaoni baada ya kusambaa kwa sauti zinazodaiwa kuwa ni mazungumzo kati yake na Mama wa Msanii Wema Sepetu, kuhusu sakata la dawa za kulevya linalomkabili Wema Sepetu.
Katika hatua nyingine, Mwenyenyiki wa CHADEMA, Freeman Mbowe alifika katika kituo hicho kikuu cha polisi Dar es Salaam, na kisha kupandishwa kwenye gari ya polisi na kupelekwa kusikojulikana.
Kamishna Sirro alipoulizwa kuhusiana na kinachoendelea kwa mwenyekiti huyo, alisema kuwa jeshi hilo lina mamlaka ya kumuita Mbowe wakati wowote kwa ajili ya mahojiano.
Msikilize hapa akifafanua baada ya kuulizwa maswali na waandishi wa habari