Walau kidogo watu wanaweza kupumua, hii ni baada ya taarifa kutoka kuwa mpiganaji Conor McGregor na bondia Floyd Mayweather wanaonekana kukaribia kuingia ulingoni.
Ingawa hakuna mkataba rasmi uliosainiwa, jarida la Irish Sun linaripoti kuwa mpiganaji huyo kutoka kwenye kampuni ya upiganaji ya Ultimate Fighting Championship (UFC) na bondia aliyestaafu wanaonekana kukaribia kufikia makubaliano ya kiuchumi ili kufanya mchezo huo ufanyike ambao utakuwa ndondi. Ripoti inasema kuna upande wa tatu ambao unafanya mkataba huo usisainiwe.
Kama tunaweza kumuamini rais wa UFC, Dana White mambo yanaweza kwenda mrama kati ya mapromota na mtukutu McGregor.
McGregor ama “Notorious” hajawahi kuficha kuwa siku zote anafanya mambo kwa misingi yake mwenyewe.
McGregor amekuwa anatamani kupata hili pambano kwa udi na uvumba lakini likiwa na fedha pia. Mwishoni mwa mwaka jana, McGregor alipata leseni ya kushiriki mchezo wa ndondi katika jimbo la California. Lakini pia alitoa video zilizomuonyesha kifanya mazoezi ya ubondia maarufu kama Sparring.
Mayweather siku zote amekuwa muwazi kuwa haogopi kupigana na “Notorious.” Katika siku za karibuni alimwambia Jim Gray kwenye mahojiano maalumu kuwa mpambano wake na McGregor upo kwenye hatua za mwisho za kuiva.
Mpambano wa mwisho wa McGregor ulikuwa dhidi ya Eddie Alvarez kwenye UFC 205 ndani ya Madison Square Garden huko katika jiji la New York. “Notorious” alimpiga Alvarez ukiwa ni ushindi wake wa pili wa TKO. Ushindi huo ulimfanya McGregor kuwa mtu wa kwanza kushinda mikanda miwili ya UFC kwa nyakati zilizofuatana.
Mayweather ameonekana ulingoni mara ya mwisho Sept. 2015.