SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 15 Februari 2017

T media news

KILICHOTOKEA PSG VS BARCELONA. UCHAMBUZI

Mara ya mwisho Barcelona kuondolewa kwenye hatua ya 16 ilikuwa dhidi ya Liverpool, miaka kumi iliyopita. Inawezekana kabisa hata sasa safari ikawa imeiva, Inawezekana kabisa hata wao rohoni wakawa wamepata kitu cha kuelewa juu ya udhaifu wao. PSG dhidi yao walikuwa ni Golliath ambao walipambana na Daudi ambaye hakuwa na lile jiwe hivyo asingeweza kuwa na msaada kama ilivyoandikwa kwenye maandiko matakatifu. Walizidiwa katika kila nafasi na hata kimavazi Unai Emery alionekana kuwa bora zaidi. Sikuona wapi ambapo Barcelona walivutia kwenye mchezo wa jana.
RABIOT 

Huyu aliingia kuchukua nafasi ya Thiago Motta. Alifanya kila kitu sawa, akaamua kufanya na ya ziada. Alimfanya Busquet aonekane anajifunza soka. Aliamua timu icheze vipi na alishurutisha kila kitu na mfumo na timu kwa ujumla vikatii. Inawezekana akalazimisha kuwa mhimili wao wa moja kwa moja. 

VERRATTI

Huyu anaitwa remote control. Sauti ikizidi upinzani anapunguza. Wakicheza vibaya anabadilisha kituo cha kutizama. Mpira ukikosa pa kwenda anapatiwa yeye kwa sababu atahakikisha unaenda sehemu salama ambayo sio nje wala kwa adui. Inawezekana akasababisha hata mpira wa adhabu. Hii ndiyo kazi yake kubwa. Wala akuhitaji kushambulia sana kwa sababu Rabiot alipewa uhuru huo akitokea katikati. 

MATUIDI 

Gari ilianzia safari miguuni mwake. Alivaa kitambaa cha unahodha na akawa kiongozi. Huyu aliamua timu ikabe vipi wakati wapinzani wanashambulia. Aidha watumie nguvu ama wacheze taratibu. Ni huyu ambaye alikuwa anawapa uhuru Di Maria na Draxler kwa sababu anaweza kwenda eneo lolote na kuhakikisha usalama. Hivyo alirahisisha kubadilishana kwao kwa nafasi. 

KWANINI HAWA WATATU?
Hawa ndio waliamua mchezo wa jana. Ukitaka kuimaliza Barcelona maana yake ifanye MSN isipate mipira sahihi. Lucas Moura kabla ya mchezo huu alisema namna pekee ya kumzuia Messi ni kuhakikisha hapati mpira. Hii ndio sababu kadi nyingi za njano zimetoka jana. PSG waliamua kufanya kazi na wa kwanza kabisa kuingia kitabuni alikuwa Rabiot. Walifahamu fika kuwa Wakicheza kwa namna ambayo Barcelona wanataka na kuwapa nafasi basi dhahama ilikuwa inawakumba. 
Lakini kama hiyo haitoshi, kwa mfumo wa PSG wa 433, maana yake walifanana kila kitu na Barcelona kwa maana ya staili ya uchezaji. Hivyo ilikuwa rahisi kuhakikisha kuwa Iniesta,  Busquests na Gomez hawafanyi watakalo. Unai Emery akahakikisha kuwa hawapati mipira rahisi ambayo ingeweza kuwaruhusu kuisogeza timu mbele na kuwapa vyumba vya kuwa na uhuru Suarez, Messi na Neymar. Hivyo mchezo wa jana uliamuliwa na eneo hili la kiungo hata kama wachezaji walifunga kwa juhudi zao.
INAMAANISHA NINI KWA BARCELONA. 
Kwa kipindi kirefu Barcelona waliishi kwa amani kwa sababu ilikuwa nadra kuona eneo lao la kiungo likizamishwa kwenye kina kirefu. Lakini Iniesta sio yule tena. Ametumika sana, na alichobakisha kwa kiasi kikubwa ni ubunifu na sio workrate uwanjani. Hawezi kukimbia umbali mrefu kwa kiasi kikubwa tena. 

Gomez hawezi kuwa mrithi wa Xavi na bahati mbaya hawezi kufanya kazi aliyokuwa anaifanya Rakitic ambaye muda mwingi misimu miwili iliyopita alikuwa akihakikisha kuna muunganiko kati ya Busquests na Iniesta. Alifanya kazi kubwa. Lakini pia Busquet hakuwa na akili yake jana. Huyu ni moja kati ya viungo ambao wanafahamu namna ya kuusoma mchezo na kuutolea majibu, lakini jana hakuwa jirani na ukweli wowote. 

UNAI EMERY. 

Kocha huyu aliletwa na fedha za waarabu kuhakikisha jambo moja tu, UEFA inapatikana heshima. Na ndicho kinachotokea. Hawatumii nguvu nyingi kwenye ligi na huku wanaweza kuwa hatari sana. Wakati huu ambao jinamizi la Zlatan limeondoka kichwani kwa Cavani na ongezeko la Draxler linawafanya PSG kuwa wepesi zaidi kwa  maana ya kubadilishana nafasi na kuhakikisha kuwa wanalinda maeneo mpira unapoweza kupita vyema. Hii ni silaha yao kwa sasa na vilabu vingi vitapata shida kuzuia hili.
MARQUINHOS NI KIONGOZI 

Hakuwepo Thiago Silva lakini huyu Kijana alionyesha ni kwanini safu ya Ulinzi ya Brazil inajengwa kupitia yeye kwa sasa. Mtulivu na anajua namna ya kuzungumza na wachezaji wenzie. Alimtuliza vyema Kimpembe na mabeki wa pembeni Kurzawa na Muenier. Safi sana.
Nyakati zimesogea na hizi ni siku chache kati ya zile nyingi ambazo ungeweza kuikuta Barcelona haiwezi kufanya lolote. Lakini wana kazi kubwa ya kufanya. Eneo la ulinzi lipo wazi, na unaweza kuhisi baadhi ya wanadamu wana bahati kwani PIQUE anacheza mwaka wake wa 9 sasa pamoja na siku zote kukosolewa zaidi. Lakini Umtiti naye haonekani kama anafanana na timu hiyo. Hongera PSG

By Nicasius Agwnada (Coutinho)

Insta @kotinyotz