Inawezekana mpaka leo unalalamika ya kwamba maisha yako yamekuwa katika wakati mgumu, inawekana umekata tamaa, inawezekana pengine huna matumaini ya kufanikiwa, ila nataka kukwambia ya kwamba usiwe katika hali hiyo kwani Mwenyezi Mungu ana kusudio lake la wewe kuwepo katika dunia hii, hivyo nikusihi ya kwamba ni vyema akaendelea kila wakati kuendelea kusoma elimu mbalimbali kuhusu mafanikio ili uweze kufanikiwa. Kwa leo tutangalia jambo lifuatalo.
Ili kutimiza malengo yako unahitaji kuweza kuyafuata mambo yafuatayo;
1.Kuchagua
Mwanadamu yeyote mwenye haki ya kuishi hapa dunia ana hitaji upeo wa hali ya juu sana ili kufanikiwa, haiwezekana kabisa ukasema unahitaji mafanikio harafu ukashindwa kuchagua kile kilicho chema kwako. Maisha ya wengi yamekuwa mashakani kwa sababu wengi wetu tumeshindwa kuchagua vitu sahihi vya kufanya. Hivi hujawahi kuona mtu analalamika ya kwamba biashara ngumu? Bila shaka utakuwa umewahi kuonana na watu wa aina hii, lakini ukifanya uchungizi wa kina juu ya jambo hili utagundua ya kwamba mtu huyo halikuwa chaguo lake kufanya biashara hiyo, ila alifanya baada ya kuona mtu fulani anafanya biashara hiyo.
Suala ya kutofanya uchaguzi sahihi si kwa mfanyabiashara tu, ila suala la watu wengi kushindwa kufanikiwa mara nyingi hutokana na kushindwa kuchagua mambo ambayo ni chaguo lako. Hapa ndipo ambapo nakumbuka ule usemi ambao husema ya kwamba Ni heri ukosee njia ya kupita ila si kukosea kuchagua mke Wa kuoa. Kama ilivyo katika usemi huo nami nasema ya kwamba kama tutashindwa kufanya uchaguzi wa vitu vya kufanya ama hakika tutakufa maskini huku tukiziacha Ndoto zetu kubwa ziweze kupotelea hewani.
Hivyo kwa kuwa wewe ni mwenye mamlaka ya kutaka kuona unatimiza malengo yako, hakikisha ya kwamba unafanya mambo ambayo umeyachagua mwenyewe, na si kufanya jambo kisa mtu mwingine anafanya au kwa sababu mtu mwingine amekwambia ufanye. Kwani endapo utachaguliwa jambo la kufanya hautalitenda kwa ufasaha.
2.Uhuru (freedom)
Baada ya kufanya uchaguzi wa jambo ambalo unalitaka kulifanya, jambo la pili unahitaji uhuru Wa
Kutenda jambo hilo. Uhuru ambao ninauzungumzia ni kwamba huwezi kufanya jambo fulani kwa ufasaha kama huna uhuru. Ni heri kupata hata kitu kidogo kwa uhuru kuliko kupata kingi kwa mateso au manyanyaso. Kama unafanya biashara hakikisha unachagua eneo ambalo utaifanya biashara hiyo kwa uhuru bila manyanyaso yeyote. Wengi ya watu tumekuwa tukifanya mambo mbalimbali kwa wasiwasi, kufanya hivyo ni kujidanyanya wenyewe. Kama unataka kufanikiwa chagua kitu sahihi na chagua kitu ambacho utakitenda kwa Uhuru usiokuwa na kikomo.
3. Uwajibikaje.
Hakuna mafanikio ya kweli kama utayafanya yote ambayo nimeyatabainisha hapo juu na ukashindwa kulifanyia kazi hili la tatu, kwa jambo lolote ambalo umelipanga kulifanaya unahitaji kuweza kulitekeleza kwa kiwango cha juu sana, haiwezekani ukawa mvivu harafu ukategemea eti ndoto zako zitakuwa kweli.
Ukiwa uvivu habari za kufanikiwa zitakuwa ni ngumu sana. Unachokihitaji ni kuwekeza muda, mawazo, akili pamoja na nguvu katika kutekeleza jambo ambalo umelikusudia. Ukifanya hivyo itakuwa ni njia rahisi ambayo itakufanya uweze kufanikiwa.
Kwa leo naomba niweke nukta kwa kusema nakutikia siku njema na Mafanikio mema. Tukutane tena siku nyingine.
NAAMINI KTK KUJIFUNZA
Imeandikwa na Afisa Mipango Benson Chonya
bensonchonya23@gmail.com