Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba jana alikuwa katika wakati mgumu kueleza sababu za kuonekana mara kwa mara katika shughuli za kiserikali kuliko zile zinazohusu vyama vya upinzani.
Profesa Lipumba ambaye ana mgogoro na chama chake, alikuwa katika kipindi cha Funguka kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Azam TV akiwa na mtangazaji mkongwe, Tido Mhando.
Akijibu swali hilo, Profesa Lipumba, ambaye licha ya kuvuliwa uenyekiti wake bado anatambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, alisema kuonekana kwake kwenye shughuli hizo kusichukuliwe kuwa yuko karibu na Serikali, bali huo ni utamaduni aliojiwekea muda mrefu.
Profesa Lipumba alisema hawezi kukataa kuhudhuria shughuli za Serikali kwa kuwa anatoka chama cha upinzani, sababu maendeleo hayana chama.
“Kama nimealikwa katika shughuli ambayo Rais anafungua miundombinu yenye manufaa kwa Taifa zima, siwezi kuacha kwenda. Nitahudhuria, nitakwenda tu kwa sababu maendeleo hayana chama.
“Sijaanza juzi kuhudhuria shughuli za kiserikali. Ukifuatilia utagundua kuwa huo ni utamaduni wangu tangu zamani. Nikialikwa katika shughuli za kiserikali na nikiwa na nafasi nimekuwa nikihudhuria,” alisema.