Wakati zikiwa zimesalia saa chache upigwe mchezo wa Simba vs Yanga ambao unasubiriwa na maelfu ya wapenda soka kwenye pembe mbalimbali za ulimwengu,shaffihdauda.co.tz inakuletea exclusive ya nahodha wa Yanga Cannavaro ambaye kwa upande wake amemtaja mchezji ambaye amewahi kumsumbua kwa muda mrefu zinapokutana timu hizi mbili zenye historia ya aina yake kwenye soka la Bongo.
Beki mkongwe kwenye kikosi cha Yanga Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amesema, katika muda wote aliocheza ligi kuu Tanzania bara hakuna mchezaji ambaye amewahi kumnyima usingi kuelekea mechi ya Simba na Yanga kama mganda Emanuel Okwi.
“Kuna wachezaji wengi wazuri nawaheshimu, lakini kwa upande wa washambuliaji wapinzani, nilikuwa namheshimu sana Emanuel Okwi,” anasema Cannavaro nilipofanya nae mahojiano mwishoni mwa mwaka uliopita huko mkoani Shinyanga.
“Lazima tuseme ukweli, Okwi yuko vizuri na mara zote tukiwa tunacheza na Simba tunajua tunaenda kukutana na mtu hatari. Kwangu mimi Okwi ni professional ambaye anajitambua, ni mchezaji ambaye ukimwachia anakudhuru.”
“Ana-peed halafu ni mjanja, ni mchezaji mwenye maamuzi ya haraka. Naweza kuwa nafikiria hapa anavyokuja mimi natakiwa kufanya kitu flani lakini yeye anafanya kitu anachokifikiria kabla mimi sijafanya kitu nachokifikiria.”
“Kwa mfano, kuna goli alitufunga akiwa katikati ya uwanja (Simba 1-0 Yanga) sisi tulikuwa tunafikiria hawezi kufunga kutokanana na umbali aliopo lakini kwa sababu ni mchezaji wa kimataifa anajua nini anafanya na akatufunga. Namheshimu.”
Kwa upande wa washambuliaji wazawa, Cannavaro anasema, Jerry Tegete ni mshambuliaji wa kiwango cha juu kuwahi kuchezanae kwenye timu kwa sababu hana mambo mengi zaidi ya kuweka kambani.
“Wapo wengi wazuri, naweza nikamtaja Jerry Tegete, si mchezaji hodari sana lakini analijua goli, ni mchezaji ambaye namuheshimu na alikuwa anajua sana kufunga.”
Kwa sasa kiwango cha Tegege kimeshuka kwani hata kwenye kikosi cha Mwadui ambacho ndipo yupo kwa sasa baada ya kutoka Yanga, ameshindwa kupata nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza kuanzia kwa kocha Julio hadi sasa Ally Bushiri.