BILA shaka u-mzima wa afya, kaka yangu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda. Pole kwa shughuli nzito ya ujenzi wa Taifa uliyonayo. Mimi ndugu yako ni mzima wa afya, namshukuru Mungu. Naendelea kupambana kwenye eneo langu,
Ndugu yangu leo nimekukumbuka kwa barua. Nimeona si vyema vuguvugu hili la madawa ya kulevya likapita hivihivi bila mimi kuzungumza jambo na wewe. Kwanza nakupongeza. Umeonesha uthubutu wa hali ya juu.
Kwa vijana wa mtaani wanasema umejilipua. Si siri inahitaji ujasiri mkubwa sana kufanya jambo unalolifanya, ndiyo maana wengi wetu tumekuwa tukiishia kusema tu chinichini kwamba fulani anauza, fulani anatumia madawa ya kulevya lakini si hadharani.
Ndugu yangu mimi naona kwa ulichokifanya, kinapaswa kuungwa mkono na mtu yeyote kwa kuwa dhamira yako ilikuwa njema. Hata kama watu wameibuka na kukupinga, kuibua ‘madudu’ wanayoyajua lakini mwisho wa siku lazima tukubaliane tu, wewe umeonesha kwa vitendo kwamba unapaswa kuwa kiongozi.
Vita uliyoiingia, imewashinda wengi. Hawa ambao wanaibuka sasa hivi na kukosoa mfumo unaotumia, wengi wao walikuwa wanafahamu madhara ya madawa ya kulevya lakini kwa sababu wanazozijua, walifunga midomo yao. Mbunge wa Geita vijijini, Joseph Kasheku Msukuma (CCM) yawezekana alikuwa na hoja zake za msingi katika kukukosoa, lakini niliona ni vyema nguvu zake angezielekeza zaidi kwenye kukushauri na si kuibua yale ya utajiri wako na mambo mengine.
Niliona ni busara hayo ya utajiri, pengine angeyaibua kabla au hata baada ya sakata hili kupita kuliko kuliibua katika kipindi ambacho wewe unatupa silaha zako katika kupambana na madawa ya kulevya. Ongeza nguvu zaidi kaka, tuko nyuma yako.
Wewe umefanya, wengi wao wametutoa kwenye hoja ya msingi na kutupeleka kwenye hoja binafsi. Wanataka kutulisha mambo binafsi,
tusahau tatizo la msingi. Nikwambie tu mkuu wangu wa mkoa, usikate tamaa, songa mbele. Pale ambapo unaona kunatolewa ushauri wa msingi kuhusu vita hii, ni vyema ukauchukua na kuufanyia kazi.
Tunakubaliana kwamba katika kusaka suluhu ya jambo, si rahisi kusikiliza kila mtu lakini kwa kuwa nawe ni kiongozi, hakika unao upeo wa kutosha wa kung’amua mambo.
Tangu sakata hili limeanza, nimejaribu kufuatilia, wapo watu wengi sana ambao wamekuwa wakishauri mambo ya msingi ambayo hata mimi naamini ukiyasikiliza, bado yataongeza tija. Mfano ni lile suala la kuwashughulikia kimyakimya, linaweza likatoa majibu chanya pia.
Kaka, una jeshi la polisi ambalo lipo chini yako, endelea kulimulika nalo kwani maneno ya kwamba wao ndiyo sehemu kubwa ya tatizo yanasemwa sana huku mtaani. Ni lazima uwe na askari juu ya askari. Wachungazane wenyewe kwa wenyewe, usimuamini mtu mmoja. Tuwe na askari waaminifu, watakaoweza kweli kutokomeza vijiwe vyote vya mitaani ambavyo vinajulikana hata kwa watoto wadogo kwamba sehemu fulani kunauzwa unga. Doria zifanyike mara kwa mara, wenyeviti wa mitaa kweli washiriki kikamilifu katika vita hii maana wao wanawajua watu wao.
Lengo letu ni moja, sidhani kama unaweza kukataa kupokea ushauri ambao nao una lengo la kujenga. Tunaamini kwa gia yako ya awali, unaweza pia kubadili gia ya pili kama hiyo ya kimyakimya na mambo yakaenda vizuri. Ni matumaini yangu utakuwa umenielewa na nikutakie kila la kheri katika mambo haya mazito ambayo umeyaanzisha.s
Mimi kama kijana mwenzio, nakuombea kwa Mungu, akupe ulinzi wake na uweze kutekeleza vyema wajibu wako hapa duniani kwa nafasi ambayo Mungu amekupa. Mimi ni ndugu yenu;
Erick Evarist