KUPOROMOKA kwa sarafu ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani kwa takribani asilimia 15 ndani ya mwezi mmoja, kumeonesha kuwashtua baadhi ya wachumi ambao wanasema huenda ukatokea mfumuko wa bei.
Wakati hali ikiwa hivyo mijadala mizito imeibuka katika mitandao ya kijamii mbalimbali kuhusu kuporoka huko kwa Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani.
Kutokana na hali hiyo Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu, ambaye alikiri kuwapo kwa hali hiyo na kusema ofisi yake imeanza kushughulikia suala hilo kuhakikisha mporomoko huo unatengemaa kabla hayajatokea madhara makubwa.
Kwa sasa katika maduka mbalimbali ya kubadilishia fedha, jijini Dar es Salaam Dola moja ya Marekani inanunuliwa kwa kati ya Sh 2,270 na Sh 2, 290 kutoka Sh 2,180 mwanzoni mwa Januari mwaka huu.
Kwa mara ya mwisho katika miaka ya karibuni, shilingi iliporomoka zaidi Juni mwaka 2015 ambapo Dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa Sh 2,400 na baada ya BoT kuingilia kati ilishuka na kufikia Sh 1,967.
“Sisi kazi yetu ni kujaribu kutafuta utulivu (wa soko la fedha), kuna mambo yanasababishwa na ya nje, kuna mambo ambayo tunaweza kufanya sisi, hivi ninavyokueleza nia yetu ni kuhakikisha panautulivu na tunachukua hatua kwa madhumuni hayo,” alisema.
Alipoulizwa athari za kushuka kwa shilingi, Prof. Ndulu, alisema. “Hiki kitu kimetokea kwa muda mfupi hapa, tunajua namna tunavyotaka kudhibiti kwa hiyo kama itakaa kwa muda mfupi athari sijui kama zitakuwepo kwa hiyo subirini tufanye hiyo kazi,” alisema .
Alisema kwa sasa wanafanya juhudi za kuleta utulivu kutokana na mporomoko huo wa shilingi dhidi ya Dola ya Marekani huku akikataa kueleza mikakati hiyo kwa undani kwa sababu za kiufundi.
“Siyo kuuondoa (ushukaji wa shilingi) ni kwamba tutafanya juhudi zile zinataka kuleta utulivu, ndiyo kazi yetu, sasa tunafanya nini haswa hapa, hiyo itakuja kutuharibia shughuli yetu tusifanye sawasawa, hatufanyii magazetini,” alisema.
Mwandishi alipomwuliza hatua ya kupanda huko kwa dola kama kunaweza kuathiri deni la Taifa la nje na la ndani, Profesa Ndulu alisema kama haijafika tarehe ya kulipa hayawezi kutokea madhara ya aina yoyote ila kwa siku husika ya malipo ndiyo inaweza kuwa hivyo kama dola itabaki kama ilivyo sasa.
“Sikia hii valuation (hesabu) unaweza kuifanya siku yoyote lakini madhara yake kama kutokea yanatokea unalipa, kama haijafikia tarehe ya kulipa itakupaje madhara? Labda tarehe ya kulipa haitakuwa (dola) huko juu itakuwa iko chini ndiyo ukweli,” alisem Profesa Ndulu.
Wataalamu wachambua
Wakizungumzia hatua hiyo baadhi ya wachumi walisema hali hiyo inaweza kusababisha mfumuko wa bei, jambo litakalo athiri moja kwa moja wananchi.
Mhadhiri wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Haji Semboja, alisema kuporomoka kwa shilingi ni kiashiria kwamba mahitaji ya dola kwa Watanzania yameongezeka kwa kiasi kikubwa.
Alisema hali hiyo itasababisha madhara ya kiuchumi kwani fedha nyingi zitalazimika kutolewa huku zitakazoingizwa zikiwa chache.
“Kuna kupanda kwa uchumi na kushuka kwa uchumi, tusipaniki tuwe waangalifu tusiliingilie soko kwani tunaweza kuleta madhara zaidi, lazima tujue dunia inakwendaje,” alisema Profesa Semboja.
Hata hivyo alisema hali hiyo ya kuporomoka kwa shilingi inaweza ikadumu kwa muda mfupi au ikaongezeka hadi mwezi Machi kama mvua hazitanyesha.
Profesa Moshi
Mhadhiri wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Humphrey Moshi, ameainisha sababu kadhaa zilizochangia kuporomoka kwa shilingi kuwa ni pamoja na ukame na kupungua kwa kasi ya uwekezaji.
“Inawezekana uagizaji umeongezeka lakini uzalishaji wa shilingi umepungua na inawezekana jinsi kulivyo na ukame mazao ya kupeleka nje yamepungua. Pia kunaweza kuwa na utoroshaji wa fedha kwenda nje.
“Tulitegemea wakati huu ambapo safari za watumishi kwenda nje zimepungua mahitaji ya dola yangekuwa machache lakini inashangaza kwamba hali imebadilika kiasi hiki,” alisema Profesa Moshi.
Pia alisema wawekezaji ambao walitaka kuweka fedha zao ndani wanaweza kuona sera hazijakaa sawasawa wakaamua wasiwekeze kwanza wasubiri.
Alisema hali hiyo itasababisha madhara ya kiuchumi kama vile kuongezeka kwa mfumuko wa bei hasa katika vyakula.
“Huko tuendako tunaona hali ya chakula si nzuri na kuna uwezekano kikaagizwa zaidi kutoka nje hivyo, hali ya maisha itazidi kuwa mbaya kwa sababu gharama zitaongezeka wakati uzalishaji hauongezeki,” alisema.
Profesa Moshi alishauri viwanda visukumwe vizalishe badala ya kuagiza vitu kutoka nje ili kupunguza mahitaji ya dola.
“Wataalamu wa ndani tukizungumza hatusikilizwi hadi waje wataalamu wa nje lakini tunasema kila siku ni lazima tuwekeze kwenye kilimo cha umwagiliaji. Tuna maziwa makubwa ya kutosha na tunaweza kujitegemea kwa chakula na kulisha nchi nyingine,” alisema.
Kafulila
Naye mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), David Kafulila, ambaye pia kitaaluma ni mchumi, alisema athari za kuporomoka kwa shilingi ni kubwa kwa malipo ya nje pamoja na deni la taifa kuongezeka.
Akifafanua alisema mwanzoni mwa mwezi huu deni la nje ambalo lilikuwa Sh trilioni 35.67 sasa limefikia trilioni 37.556 kutokana na kuyumba kwa shilingi.
“Shilingi ya Kenya imeyumba kwa asilimia 1.76 lakini shilingi yetu imeyumba kwa asilimia 5.28 na sababu ya kushuka kwa kasi zaidi mbali na kupungua kwa uuzaji bidhaa nje pia kukwama kwa misaada na mikopo kumechangia,” alisema Kafulila.
Baadhi ya bidhaa zinazoagizwa nje ya nchi ikiwa ni pamoja na nishati ya mafuta kama shilingi itaendelea kuporomoka bidhaa hiyo huenda bei yake ikapaa mara dufu jambo ambalo linaweza kuleta madhara kwa wananchi.