MAKAMU wa Rais wa Benki ya Dunia (WB) kwa upande wa Afrika, Makhtar Diop, ameipongeza Serikali kwa kufanikiwa mradi wa mabasi ya mwendokasi, huku akisema baada ya miaka 25 Jiji la Dar es Salaam litafikisha watu milioni 10, hivyo upanuzi wa miundombinu ni muhimu.
Diop aliyasema hayo jana Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa awamu ya kwanza ya mradi wa mabasi yaendayo haraka (DART) uliofadhiliwa na Benki ya Dunia.
“Mji wa Dar es Salaam una idadi ya watu milioni tano na kwa miaka 25 ijayo kutakuwa na idadi ya watu milioni 10. Kwa hiyo ni jambo zuri na la kupongeza kwa Serikali kuweka miundombinu bora ya usafirishaji kama hii. Pia itakuwa vizuri zaidi kwa kuweka usafiri wa majini kama feri ili kuwe na mwingiliano kwa mtu kuunganisha usafili ili kuwahi kwenye shughuli zake,” alisema Diop.
Alisema mradi wa mabasi ya mwendokasi ni sehemu ya mabadiliko ya Jiji la Dar es Salaam, hivyo utachochea maendeleo na kubadili tabia za wananchi.
“Kutokana na mradi huu, majengo ya kibiashara, ofisi na makazi yataendana na hadhi na mandhari ya mabadiliko ya mji huu. Kwetu Senegal hatuna mradi kama huu, lakini natumaini siku si nyingi nasi tutakuwa nao,” alisema.
DART
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa DART, Mhandisi Ronald Lwakatare, alisema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ilianzisha mpango wa kuwa na mradi wa mabasi yaendayo haraka mwaka 2003.
Lwakatare alisema mpango huo uliendelea na ilipofika mwaka 2007, Serikali ikaupitisha, hivyo mwaka 2010 ujenzi wa barabara za BRT ukaanza.
Alisema kwa sasa taratibu za kumpata mtoa huduma za kudumu za mradi huo zinaendelea kwa kushindanisha wazabuni.
Aliongeza kwa kusema wakati huduma za mabasi yaendayo haraka zinaanza, walikusanya zaidi ya Sh milioni 800 kwa mwezi, kwa sasa makusanyo hayo yameongezeka na kufika Sh bilioni 3.39.
TANROADS
Awali Mkurugenzi wa Miradi wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mhandisi Crispianus Ako, alisema lengo la kuanzishwa kwa mradi huo ni kupunguza msongamano wa magari.
Aliongeza kuwa barabara za BRT zimejengwa kwa kiwango cha zege na kokoto na zitadumu kwa miaka 40 bila matengenezo makubwa.
SIMBACHAWENE
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa -TAMISEMI, George Simbachawene, alisema mradi huo umeajiri wananchi 962 na kwamba kwa sasa unasafirisha zaidi ya watu 200,000 kila siku.
“Mradi huu umeajiri wananchi 962, idadi hii inajumuisha madereva, na wafanyakazi wengine wote, pia kuanzishwa kwa mradi huu kumenufaisha wananchi kibiashara ambapo baadhi wameanzisha sehemu za maegesho ya magari. Kwa mantiki hiyo kuwapo kwa mradi huo ni kichocheo kikubwa cha uchumi wa wananchi,” alisema.
Aliongeza pia kuwa kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi huo, kunaifanya Tanzania kuwa nchi ya tatu kwa kuwa na mradi wa mabasi yaendayo haraka Afrika.
“Nchi ya kwanza kuwa na mradi kama huu ni Nigeria ambao wanabeba watu elfu 62 kwa siku, nchi ya pili ni Afrika Kusini ambao wanabeba watu 200,000 kwa siku na sisi Tanzania ni wa tatu na tayari tunabeba abiria zaidi ya 200,000 kwa siku na mpaka miradi yote sita ikikamilika, jumla ya watu 450,000 kwa siku watakuwa wanabebwa kwenye mabasi yaendayo haraka,” alisema Simbachawene.