SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 16 Desemba 2016

T media news

Ikiwa waamuzi, makocha, wachezaji na bodi ya ligi watafanya haya, VPL itakuwa bora

Na Baraka Mbolembole

LIGI Kuu Tanzania Bara (Vodacom Premier League) inataraji kuendelea tena siku ya kesho Jumamosi na siku ya Jumapili hii.

Michezo minne itachezwa kesho katika miji ya Dar es Salaam JKT Ruvu v Yanga SC, Mbeya City FC v Kagera Sugar FC, Ruvu Shooting v Mtibwa Sugar FC na Mwadui FC v Toto Africans.

Siku ya Jumapili, African Lyon itacheza na Azam FC katika uwanja wa Uhuru, Tanzania Prisons v Majimaji FC, Ndanda FC watakuwa wenyeji wa Simba SC na mchezo mwingine utawakutanisha Mbao FC v Stand United katika uwanja wa Kirumba, Mwanza.

Katika mzunguko wa pili ningependa kuona…

WAAMUZI  

Bila shaka waamuzi ndio ‘mabosi wa dakika 90’ za mchezo wa kandanda, lakini kila mara wamekuwa wakilaumiwa kutokana na maamuzi yao.

Kuna waamuzi kadhaa wameondolewa na kufungiwa na Shirikisho la soka nchini-TFF kutokana na uchezeshaji wao kuonekana hauridhishi katika michezo ya mzunguko wa kwanza.

Nadhani huu ni wakati wao wa kurudisha imani iliyopotea dhidi yao kiasi cha kufikia klabu ya Simba SC kusema hadharani hawataingiza timu yao uwanjani kucheza na mahasimu wao Yanga ikitokea TFF ikawapanga waamuzi wa Tanzania.

Ni kweli waamuzi nao ni  binadamu, hivyo wanapaswa kukosea ila hawapaswi kuwa dhaifu katika kutoa maamuzi wanayoona ni sahihi na kuyasimamia. Haitapendeza kuona VPL ikipata bingwa atakayetokana na uamuzi mbovu wa waamuzi.

Kama timu zimejiimarisha kwa kutumia pesa na muda wao kufanya usajili, waamuzi nao wawe fair katika uchezeshaji wao licha ya kwamba kuna makosa ya kibinadamu yatajitokeza.

MAKOCHA

Yanga, JKT Ruvu, Mwadui FC, Tanzania Prisons, Ruvu Shooting  na Ndanda FC zimewasaini makocha wapya. Huu ni walati ambao tunahitaji kuona kazi ya makocha.

Ningependa kuona timu zao zikicheza vizuri na mifumo inayoonekana wakati wa kushambulia na kuzuia. Tunahitaji kuona mbinu zao za kusaka ushindi, soka la ushindi na lenye malengo.

Mzambia, George Lwandamina ambaye amechukua nafasi ya Hans van der Pluijm katika timu ya Yanga na Ally Bushiri aliyej iunga na kikosi cha Mwadui FC ndiyo maingizo pekee mapya katika VPL msimu huu, makocha wengine ni walewale waliozoeleka japokuwa wengine wamebadilisha timu tu.

WACHEZAJI

Umefika wakati wa wachezaji wa timu za ligi kuu kucheza huku wakikimbia uwanjani, kupiga pasi zenye nguvu na zinazofika kwa walengwa, kucheza kwa kufuata maelekezo ya benchi la ufundi na maarifa binafsi kwa ajili ya kuzibeba timu zao.

Kasi ndani ya uwanja ndio hufanya mchezo kupendeza na wakati huu wachezaji wakilipwa vizuri itapendeza sana kuona wakicheza kwa nguvu na ‘kutotumika’ na timu pinzani sababu hakuna ambaye amewahi kupata mafanikio baada ya kucheza chini ya kiwango kwa faida ya timu pinzani.

RATIBA

Bodi ya ligi imetoa ratiba yote ya michezo ya mzunguko wa pili hivyo haitapendeza kuona ratiba hiyo ikivurugwa mara kwa mara japokuwa ni lazima baadhi ya michezo italazimika kusogezwa mbele kutokana na ushiriki wa vilabu vya Yanga na Azam FC katika michuano ya Caf mapema mwakani.

TFF pamoja na bodi ya ligi wanapaswa kufahamu marekebisho ya mara kwa mara ya ratiba huzivuruga timu na kupunguza msisimko na ushindani.