SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 24 Novemba 2016

T media news

WASTAAFU WA TANZANIA NA WALIYOYAZUNGUMZA KUHUSU UTAWALA WA AWAMU YA TANO SOMA HAPA LIVE!!


Zikiwa zimesali siku chache kabla Serikali ya Rais Dk. John  Magufuli kutimiza mwaka mmoja tangu iingie madarakani, huku ikiwa ni miezi michache tangu akabidhiwe nafasi ya Uenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kumeanza kuibuka kauli tata zenye dalili ya kuonya, kukosoa na pengine kushauri kutoka kwa baadhi ya Wazee wenye kuheshimika ndani na nje ya chama na serikali.
Kauli za wazee hao ambao miongoni mwao walipata kushikilia nafasi za juu za uongozi ndani ya chama na ndani ya serikali, zimeibua maswali na mijadala ambayo imekuwa ikiendelea nje na ndani ya mitandao ya kijamii.
Wadadisi wa mambo wanaitaja hatua hiyo kuwa ni uamuzi wa wazee hao ambao ni Rais wa awamu ya pili Ali Hassa Mwinyi, Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete,Waziri Mkuu wa zamani Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba na aliyekuwa mtu wa karibu wa Mwalimu Julius Nyerere, Joseph Butiku kumfikishia ujumbe Mwenyekiti wa chama chao na Rais wan chi  Dk John Magufuli.
Tangu aingie madarakani Novemba 5, mwaka jana baada ya Watanzania kumchagua Oktoba 25, mwaka jana, Rais Magufuli na serikali yake yeye binafsi au wateule wake wamekuwa wakitekeleza majukumu yao kwa mfumo tofauti na ule uliozoeleka.
Alianza kazi  kwa kasi ya kutimua (kutumbua majipu)  baadhi ya watendaji waliodaiwa kuwa si waaminifu, kushughulika na wakwepa kodi wote,  pamoja na kufuta baadhi ya sherehe na safari  za nje.
Maamuzi hayo na mengine ambayo yamekuwa yakilalamikiwa pia na upinzani yameonekana kuwaibua makada hao ambao bado wanaheshima kubwa hata nje ya ulingo wa kisiasa.
Baadhi yao wanatajwa kuwa chachu ya ushindi ya Chama Cha Mapinduzi katika awamu zilizopita na hata katika awamu hii. Mara zote wanatajwa kuwa msaada mkubwa kwa CCM katika kupata ushindi hasa wa nafasi ya urais.
Kwa nyakati tofauti magwiji hao wa siasa za chama kimoja na hata hizi za vyama vingi, wametoa kauli zinazotafsiriwa na wengi kuwa ni dalili ya kutokuamini kinachoendelea ndani na nje ya chama na serikali  huku wachambuzi wa masuala ya kisiasa wakifikiri  kuwa kauli hizo ambazo hazimtaji mtu moija kwa moja zinatolewa kwa nia ya kutaka kufikisha ujumbe kwa wahusika.
Kauli za makada hawa zimeanza kutolewa kabla na hata baada ya maadhimisho ya miaka 17, ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Wadadisi wa mambo wanazieleza kauli hizo ambazo hazimlengi Rais Magufuli na Serikali yake moja kwa moja kutokana na kutumika kwa lugha ya jumla, kuwa ni za kimkakati zenye kulenga kuonya au kuelezea hisia zao kutokana na kuona baadhi ya mambo kutokwenda sawa.
Jaji Warioba ndiye alikuwa wa kwanza kuweka hadharani hisia zake, Septemba 27, 2016 akiwa katika mhadhara wa tatu wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es salaam na kusema:
“Sijui kama tuna itikadi na Sera siku hizi, tunategemea matukio na watu. Siku hizi wananchi hawajui tunaelekea wapi, zamani kulikuwa na Sera na itikadi, lakini hata ukiangalia vyombo vya habari ni siasa tu.”
Jaji Warioba katika maelezo yake alizungumzia pia nchi kupoteza mwelekeo na kuongeza kuwa vitendo vya ubaguzi kwa misingi ya vyama na ukabila sasa hivi vimekithiri .
Kauli ya Jaji Warioba ilifuatiwa na ile ya Rais mstaafu Mwinyi, ambaye siku moja kabla ya maadhimisho ya miaka 17 ya kifo cha Mwalimu Nyerere wakati akifungua mdahalo wa kumbukumbu ya Mwasisi huyo wa Taifa ikiwa ni pamoja na kuzindua kitabu cha ‘Selective works of Mwalimu Nyerere’, kilichotafsiriwa na wasomi kutoka China naye alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa mambo yanavyokwenda nchini ni kama gari lililokatika usukani.
“Mambo yanavyokwenda kama gari lililokatika usukani. Tuna utajiri wa machoni, lakini ndiyo aliyokusudia Mwalimu? Alitufundisha tuwe matajiri wa vitu au matajiri wa moyo? Tujali vitu au tujali utu?
“Siku hizi kuna panya road, wametoka wapi watoto hawa? Sisi wazee hatukuwepo? Au sisi wazee tumetengeneza mazingira kuwepo hao, mbona mwanzo hawakuwepo sasa wametoka wapi?” alihoji.
Kauli ya kuwa mambo yanavyokwenda nchini ni kama  gari lililokatika usukani inaelezwa kuzua mjadala mkubwa kwa wafuatiliaji wa masuala ya siasa huku wengi wakijiuliza mantiki halisi ya kauli hiyo kutoka kwa kada huyo mkongwe  Chama cha Mapinduzi.
Wakati kauli ya Rais mstaafu Mwinyi ikiendelea kujadiliwa, Oktoba 14, 2016 kada wa CCM na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, naye aliingia katika orodha hii kwa kuelezea umma kuwa Mwalimu Nyerere alitaka yeyote anayekuwa Rais atambue watu wote ni sawa na “usiwe wewe ni rais tembo.”
Butiku alizungumza hayo alipokuwa akiwasilisha mada ya miiko ya uongozi katika kongamano la kumbukizi ya Mwalimu Nyerere lililofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Kigamboni jijini Dar es Salaam.
“Tunachosema ni kwamba miiko ilikuwa inasema ukitaka kuwa rais utambue na uwe na imani kuwa watu wote ni sawa usiwe wewe ni Tembo,” alisema Butiku na kuongeza:
“Lazima utambue kuwa unatokana nao (watu) na lazima kiongozi huyo atambue kuwa anaongoza watu hivyo anapaswa kuwaongoza kwa heshima.”
Kauli zote hizo za makada wakongwe wa CCM, sasa zimefunikwa na kauli ya hivi karibuni ya Rais Mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Mrisho Kikwete.
Oktoba 24, 2016 akiwa katika ukumbi wa Nkurumah, wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rasi mstaafu Kikwete ambaye anatajwa kuwa na uwezo mkubwa wa kutumia misemo na nahau kufikisha ujumbe bila kumkwaza mtu, Lazima ukishakuwa mpya watu waone kuwa kuna mambo mapya, lakini mapya ya maendeleo, sio mapya ya kubomoa haya kule mlikotoka.
“Lazima ukishakuwa Kiongozi mpya watu waone kuwa kuna mambo mapya, lakini mapya ya maendeleo, sio mapya ya kubomoa haya kule tulikotoka,”alisema.
Rais Mstaafu Kikwete ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alitoa kauli hiyo kwa lugha ya Kiswahili ingawa hotuba yake yote iliandikwa kwa lugha ya Kiingereza.
Kauli yake hiyo ambayo inasambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii, imepokelewa kwa mitazamo na hisia tofauti, huku baadhi ya wafuatiliaji wa mambo wakisema kuwa alitoa kauli hiyo kwa sababu ya upya wake ndani ya uongozi wa Chuo hicho.
Kutokana na kubeba tafsiri tofauti wapo wanaosema kuwa kauli yake hiyo ambayo aliitoa na kuisindikiza na kicheko ni kama kiashiria cha kutofurahashwa na baadhi ya mambo nchini.

  – Rai