01: DIAMOND PLATNUMZ
Jina lake kamili ni Nassib Abdul, huyu wengi wamempachika jina la sukari ya warembo, idadi kubwa ya wanawake wanampenda kutokana na mwonekano wake na pia uwezo wake mkubwa wa kucheza na sauti anapoimba ingawa wengi hudai hana sauti nzuri lakini huvutiwa na namna anavyoweza kuitumia sauti hiyo na kuwa kivutio katika nyimbo zake.
Maonyesho yake hujaza watu wengi lakini inakadiriwa wasichana wengi hujitokeza katika matamasha ambayo hutangazwa kwamba msanii huyu atakuwepo, pia wengi wao hutamani kumshika msanii huyu ndiyo maana wengi wao hukimbilia kumtunza.
02: ALI KIBA
Msanii huyu anayetamba na wimbo wa ‘Mwana Dar’ na ‘Chekecha Cheketua’ jina lake kamili ni Ally Salehe Kiba, licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa kuimba na kucheza lakini wanawake wengi huvutiwa na uwezo wake wa kuchezea sauti yake katika kuimba na pia mwonekano wake akiwa jukwaani ndiyo maana mashabiki wake huwa wakimshangilia kwa sauti na kelele zote wapendavyo kila anapokuwa jukwaani.
03: CHRISTIAN BELLA
Huyu ni zaidi ya msanii kutokana na kuwa na kipaji kikubwa katika sanaa yake ya muziki, wanawake huvutiwa naye kwa sauti yake yenye mvuto wa hali ya juu na namna anavyojiweka akiwa jukwaani na pia ana uwezo mkubwa wa kucheza na mashabiki wake kiasi cha kuteka hisia za mashabiki wake.
Wanawake pia huvutiwa naye kiasi kwamba wengine humtaka zaidi ya muziki na jambo hilo alishakiri mwenyewe kwamba wapo mashabiki wake wanaomsaka kwa ajili ya kupata penzi lake.
04: YAMOTO BAND
Wasanii hawa kwa ujumla wao wamekuwa kivutio kikubwa kwa wanawake hasa wawapo jukwaani, wengi wao wameonekana kutamani kujumuika na kucheza nao jukwaani lakini wanaposhindwa wasanii hao hushuka jukwaani na kujichanganya nao hasa mashabiki wao wa kike.
Mara kadhaa wasanii wanaounda kundi hilo walishawahi kueleza kwamba wapo wanawake watu wazima huwafuatilia kwa kutaka kuwapongeza zaidi ya wanavyoimba jukwaani.
05: DIMPOZI KWA POZI
Anafahamika kama Ommy Dimpoz lakini jina lake kamili ni Omary Faraji Nyembo, wanawake huvutiwa zaidi na msanii huyu kutokana na nyimbo zake za kimapenzi ndiyo maana kila anapokuwa jukwaani humpigia kelele za kutosha.
06: MR BLUE
Msanii huyu ni wa muda mrefu asiyechuja, alipata umaarufu kwa jina la Mr Blue jina lake kamili ni Herry Sameer, ndiye msanii pekee wa hip hop anayewavutia zaidi wasichana kutokana na nyimbo zake kuwa na vionjo vya kimapenzi ambayo huwagusa zaidi wasichana.
07: BARNABA
Anaitwa Elias Barnaba, ni mmoja wa wasanii wasiobadili majina yao ya kisanii, uzuri wa sauti yake na uwezo wake wa kuimba jukwaaani na kutumia vyombo mbalimbali vya muziki ndiyo silaha yake kubwa kuwa kivutio kwa wanawake.
Mwenyewe hupenda kujiita kipenzi cha mabinti kutokana na kwamba wanawake wengi huziimba nyimbo zake mwanzo mwisho, pia ndiye msanii aliyeimba kwa ushirikiano mkubwa na wasanii wa kike ndani na nje ya nchi ambapo kwa sasa yupo mbioni kurekodi wimbo wa kushirikiana na msanii wa kike kutoka nchini Nigeria.
08: BOB JUNIOR
Ray C alifahamika kama kiuno bila mfupa na Raheem Rummy Nanji maarufu Bob Junior naye hivyo hivyo, wasichana wengi huvutiwa na kiuno chake anapocheza jukwaani, katika maonyesho yake mengi wasichana wameonekana kujaa kutokana na kuwa na mvuto naye kwa namna anavyovaa, anavyomiliki jukwaa na namna nyingine nyingi wanazovutiwa kwake.
09: JUX
Huyu ndiye mpenzi wa msanii maarufu, Vanessa Mdee, Juma Jux licha ya kuchipukia katika muziki wa Bongo Fleva lakini juhudi zake na uwezo wake wa kuchezea sauti yake, aina ya mavazi, namna anavyojiweka vimekuwa mvuto mkubwa kwa wasichana kiasi kwamba wengi wao hujikuta wakipiga kelele za kutosha katika maonyesho yake.
10: Ben Pol.
Sophia ngoma ambayo inahit hadi sasa kutoka kwa msanii Ben Pol wadada kwa wakaka wakiusikia basi inakuwa shida mpya ndani ya miyo. Msanii huyu anaongoza kwa sauti ya pekee kwenye uimbaji wa Rn'B hapa Bongo.