Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inapenda kukanusha taarifa kutoka Kwenye baadhi ya Mitandao ya Kijamii ikidai kwamba, Mhe. Kamishna wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Balozi Omar Ramadhan Mapuri (pichani) amefariki dunia.
Taarifa Rasmi ya Serikali ni kwamba taarifa hizo ni za uongo na hazina hata Chembe ya ukweli. Mhe. Kamishna Balozi Mapuri yupo hai na afya yake iko vizuri.
Mheshimiwa Balozi Omar Ramadhan Mapuri ambae kwa sasa ni Kamishna wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar alilazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa akipata matibabu na baada ya kupata huduma kutoka kwa madaktari, Mheshimiwa Balozi Mapuri aliruhusiwa kurejea nyumbani siku ya Jumamosi Novemba 12 baada ya afya yake kuimarika.
Serikali imesikitishwa na taarifa za uvumi na uzushi uliosambazwa jana na leo kwenye mitandao ya kijamii, taarifa hizi sio za kweli na tunawaomba wananchi wazipuuze.
Aidha, Serikali inapenda kuvionya vyombo vya habari na Mitandao ya kijamii kuacha kusambaza taarifa za uongo kuhusu viongozi wa Serikali.
Imetolewa na :
Dk. Juma Mohammed Salum
Kny Mkurugenzi
Idara ya Habari MAELEZO
Zanzibar