Mtu mmoja anayehusishwa na vitendo vya ugaidi, Azan Abubakary amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma Mjini na kusomewa mashtaka yake.
Akiwa amevalia fulana ya rangi ya bluu na kijani na suruali nyeusi na viatu vya matairi (maarufu kama katambuga), alisomewa shtaka lake mbele ya Hakimu Mwajuma Lukindo.
Mshtakiwa huyo anashtakiwa kwa makosa ya kufadhili ugaidi chini ya kifungu cha 13 cha sheria ya makosa ya kuzuia ugaidi namba 21 ya mwaka 2002.
Ilidaiwa kuwa Mei 15, 2016 alimtumia fedha Mohamed Ibrahim kwa njia ya M-Pesa kiasi cha Sh 265,000 katika namba +254 708104109 kwa ajili ya kufanyia ugaidi nchini.
Aidha Julai 22, 2016 Abubakary alionekana eneo la Dodoma akituma fedha kwa njia ya M-Pesa kwa Mohamed Ibrahim Sh 148,000 kwa ajili ya kufanya vitendo vya ugaidi.
Hakimu Lukindo alisema mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma katika taarifa yake kwa vyombo vya habari imesema kwamba mtuhumiwa huyo aliyefikishwa mahakamani ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Kitivo cha Afya na yupo mwaka wa pili.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, mtuhumiwa alikamatwa Nzega mkoa wa Tabora baada ya kugundulika kuwa anajihusisha na mtandao wa ugaidi wa kundi la ‘Al Shabaab’ kutoka Somalia.
Kamanda alisema mtuhumiwa alikamatwa kutokana na taarifa za Intelijensia ya Polisi katika masuala ya ugaidi.