Mkazi wa Area C mjini hapa, Boniface Kigomba amekamatwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma akiwa katika harakati za kuwaonyesha wagonjwa kliniki ya wajawazito.
Tukio hilo lilitokea jana na kusababisha wagonjwa, madaktari na wauguzi kukusanyika katika ofisi ya Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo kumshuhudia.
Hata hivyo, Polisi aliyekuwa amevalia kiraia alifika hospitalini hapo saa 8:00 mchana na kumfunga pingu Kigomba na kumpeleka kituoni.
Kigomba alikamatwa akiwa na kitambulisho cha uanafunzi cha Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) chenye namba za usajili T/DOM/2014, muhuri wa hospitali hiyo na kitambulisho kinachoonyesha ni muajiriwa wa Mfuko wa Pensheni wa LAPF.
Vitambulisho vingine alivyokutwa navyo ni cha mpigakura, uanachama wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na karatasi zilizokuwa zimeandikwa gharama za matibabu.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Caroline Damian alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakipata malalamiko kutoka kwa wagonjwa juu ya ukiukwaji wa maadili unaofanywa na mmoja wa madaktari hospitalini hapo.
“Tulimuwekea mtego siku nyingi lakini leo (jana) tuliambiwa ameonekana akiwa eneo hili ndipo tulipomkamata na kumhoji na ameonekana hakuna anachokijua kuhusiana na taaluma ya udaktari ingawa alisema yeye ni mwanafunzi wa udaktari Udom,” alisema.
Dk Caroline alisema Kagomba alipohojiwa alidai kuwa alikuwa akiwaelekeza wagonjwa eneo zinakotolewa huduma hospitalini hapo.
Alisema mbali na wagonjwa kutapeliwa fedha, hivi karibuni kumekuwa na matukio ya wizi wa vifaa.
Mwanafunzi wa Chuo cha Biashara (CBE), Tawi la Dodoma, Pafect Kadawele ambaye anaishi naye katika nyumba ya wazazi wake Area C, alisema alikutana na Kigomba miaka miwili iliyopita katika Kanisa la Upendo na baada ya kumueleza kuwa hana mahali pa kuishi aliamua kumchukua na kuishi naye.
Alisema kila siku amekuwa akimueleza kuwa anakwenda Udom anakosomea shahada ya udaktari.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema wameanza kushughulikia tatizo hilo na atatoa taarifa leo.
Makamu Mkuu wa Udom, Profesa Idrisa Kikula alisema katika orodha ya wanafunzi chuoni hapo hakuna jina linalofanana na la Kagomba.