Urambo. Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amewaasa Watanzania kutumia msiba wa Spika mstaafu, Samuel Sitta kuungana kwa kuondoa tofauti miongoni mwao.
Akizungumza juzi katika Uwanja wa Shule ya Msingi Urambo kabla ya maziko ya Sitta, Mbowe alisema licha ya tofauti za kisiasa, kidini, kikabila na kimaeneo, Watanzania wanapaswa kumuenzi kiongozi huyo kwa kujenga umoja na mshikamano katika masuala ya msingi kama alivyofanya enzi za uhai wake.
“Kuna wakati wapinzani na hata wenzetu wa CCM, tulikuwa hatuelewi msimamo wa Mzee Sitta linapokuja suala linalohitaji haki, usawa na umoja wa kitaifa kwa sababu alikuwa akiamua mambo bila kujali masilahi ya upande wowote kikiwamo chama chake,” alisema Mbowe.
Alitaka ushirikiano ulioonyeshwa na makundi yote kuanzia Serikali, vyama vya siasa na vyombo vya dola kwenye msiba wa Sitta uendelee kwa faida na masilahi ya Taifa ambayo ni ya kudumu. Mbowe aliwapongeza wakazi wa Urambo kwa heshima waliyoonyesha kwa Sitta kutokana na kujitokeza kwa wingi kumsindikiza katika safari yake ya mwisho.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri licha ya kumsifu Sitta kwa mchango wake kwa Taifa, aliwaacha hoi waombolezaji kwa kumuasa mjane wake, Margreth, kumtafuta mume mpya ambaye hatamuacha milele ambaye ni Yesu Kristo.
Mazishi ya Sitta yameacha historia kwa Mkoa wa Tabora kwa kuhudhuriwa na watu wengi kuliko yoyote yaliyowahi kutokea wilayani Urambo.