SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 17 Novemba 2016

T media news

Emmanuel Okwi ni biashara ‘kichaa zaidi’ Simba

Na Baraka Mbolembole

MIEZI 18 iliyopita Simba SC ilimuuza mshambulizi, Mganda, Emmanuel Okwi kwa ada ya uhamisho dola za Marekani 110,000 kwenda timu ya Sonderjyske ya nchini Denmark.

Akiwa amecheza mechi zisizodizi tatu kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu katika klabu yake ya sasa, Okwi amepanda thamani zaidi kufikia dola 120,000.

Ndiyo, Simba watatoa kiasi hicho cha pesa ili kumrudisha Okwi katika kikosi chao katika usajili huu wa dirisha dogo. Ni ‘biashara kichaa iliyopitiliza.’

Nasema ni biashara kichaa kwa maana, Simba italipa dola 20,000 zaidi kwa timu ya Sonderjyske wakati mchezaji huyo hana kiwango kwa sasa.

Hajacheza mechi za ushindani kwa mwaka mmoja na miezi sita sasa, jambo ambalo limechangia kukosa nafasi hata katika timu yake ya Taifa.

Ni biashara kichaa kwa maana thamani ya Okwi imepanda akiwa ‘mchezaji wa benchi’ na timu ambayo ilimnunua miezi 18 iliyopita kwa dau la dola 110,000 huku Okwi akiwa katika kiwango cha juu ndiyo hiyo imewaambia Simba walipe dola 120,000 ili kumsaini Okwi ambaye itakuwa ni mara yake ya tatu kusajiliwa na timu hiyo ya ligi kuu Tanzania Bara.

Ni biashara kichaa kwa sababu, Sonderjyske ilipolipa zaidi ya dola laki moja ili kumsaini Okwi aliyekuwa katika kiwango ilimfunga mchezaji huyo kwa mkataba wa miaka mitano, lakini Simba ambao watalazimika kutoa dola 120,000 (zaidi ya milioni 240 za kitanzania) watamsaini Mganda huyo kwa mkataba wa mwaka mmoja tu!

Tena mchezaji mwenyewe akiwa hana kiwango cha juu kama alivyokuwa wakati akiondoka klabuni hapo mara baada ya kumalizika kwa msimu wa 2014/15.

Sidhani kama Okwi ni pendekezo la wakufunzi, Mcameroon, Joseph Omog na msaidizi wake Mganda, Jackson Mayanja.

Nakumbuka mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa ‘Dar es Salaam-Pacha’ Oktoba Mosi, makamu wa rais wa klabu ya Simba, Geofrey Nyange Kaburu alinukuliwa akisema, “Kama Yanga wameshindwa kutufunga, wasahau tena kwani mbaya wao Emmanuel Okwi atarejea katika usajili wa dirisha dogo.

“Urejeo wa Okwi katika kikosi cha Simba utakuwa ni wa kishabiki zaidi kuliko kimpira kwa maana timu hiyo inapaswa kumsaini mfungaji wa magoli na hata kocha wa timu alisema hilo.

Kumsaini, Okwi ni muendelezo wa usajili mbovu na usio na faida kwa timu hiyo. Kwanini Okwi anasajiliwa kwa thamani ya juu zaidi ya ile aliyouzwa wakati hakuwa mchezaji wa mechi katika timu yake.

Kwanini, Okwi asajiliwe kwa mkataba wa mwaka mmoja wakati Denmark alisaini miaka mitano kwa ada pungufu ya inayotaka kutumiwa na Simba hivi sasa?

Huu ni usajili wa kishabiki zaidi, na itakuwa biashara kichaa zaidi kuwahi kufanywa na Simba.

Yangu macho yanamsubiri Okwi ‘asiye na makali’ ila mwenye thamani ya juu kuliko vile alivyokuwa miezi 18 iliyopita.