SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 12 Oktoba 2016

T media news

Wafuasi 22 CUF Kortini Kwa Madai ya Kukutwa na silaha za Jeshi la Polisi


Wafuasi  22 wa Kundi la ‘Blue Guard’ la Chama cha Wananchi (CUF) wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka manne likiwemo la kukutwa na silaha za Jeshi la Polisi.

Washitakiwa hao ambao ni wakazi wa Zanzibar walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali, Patrick Mwita mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa.

Mwita alidai, washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka manne ya kula njama, kuingilia majukumu ya kipolisi kupitia genge la uhalifu pamoja na kukutwa na silaha pamoja na zana za Jeshi la Polisi.

Akisoma mashitaka, Wakili Mwita alidai, kati ya Septemba 20 na 25, mwaka huu kati ya Zanzibar na Dar es Salaam, kupitia kikundi cha Blue Guard, washitakiwa na wenzao ambao hawakufikishwa mahakamani walikula njama za kuajiri watu, wafanye kazi za kipolisi kinyume cha Sheria ya Makosa ya Jinai.

Aliendelea kudai kuwa, washitakiwa wakiwa wanachama wa kundi la Blue Guard waliwaajiri watu kwa ajili ya kufanya kazi za Kipolisi kinyume na sheria.

Wakili Mwita alidai, Septemba 25, mwaka huu katika eneo la Mwananyamala, Dar es Salaam, wakiwa na lengo la kutenda kosa, washitakiwa walikutwa wakiwa na silaha kinyume cha sheria , ikiwemo visu vitano pamoja na mabomu ya machozi 10 kwa ajili ya kuyatumia katika uvamizi.

Aidha, inadaiwa siku hiyo hiyo, Dar es Salaam, washtakiwa walikutwa wakiwa na zana za Jeshi la Polisi ambazo ni mabomu ya machozi yanayotumiwa na jeshi hilo katika majukumu yao.

Baada ya kusomewa mashitaka washitakiwa hao walikana kutenda makosa hayo, hata hivyo Wakili Mwita alidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba wapangiwe tarehe nyingine ya kutajwa.

Upande wa utetezi kupitia Wakili Hekima Mwesigwa uliiomba Mahakama kuliondoa shitaka la tatu katika makosa hayo kwa sababu lina upungufu wa kisheria kwa kutumia baadhi ya maneno kupotosha.

Hata hivyo, Wakili Mwita aliiomba Mahakama kutupilia mbali maombi hayo kwa kuwa shitaka hilo halina upungufu wowote badala yake wametumia lugha ya mkato.

Hakimu Mwambapa alisema baada ya kupitia vifungu vya sheria, amebaini kuwa shitaka halina mapungufu kisheria hivyo ametupilia mbali maombi.

Aidha, alisema washtakiwa hao watapata dhamana endapo watatimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika watakaosaini hati ya Sh milioni mbili kila mmoja, pia wawasilishe vitambulisho vyao mahakamani. Kesi itatajwa tena Oktoba 20 mwaka huu.

Washtakiwa ni Hamis Omary Said (49), Said Mohamed Zaharan (57), Hamid Nassor Hemed (44), Nassor humud Ally (25), Othman Humud Abdlaah (34), Swalehe Ally Swalehe (30), Hamis Hamis Haji (46), Majid Hamis Juma (58), Mohamed Hamis Ally (34), Ramadhan Rashid Juma (30), Juma Hamad Seif (21) na Masoud Iliyasa Fumu (29).

Wengine ni Jecha Faki Juma (40), Mbaruku Hamis Bakari (31, Mohamed Alli Zuberi (43), Muhsin Ally Juma (27), Mohamed Amir Mohamed (30), Ally Juma Salum (35), Juma Hajji Mmanga (26), Ally Nassoro Ally (46), Haji Rashid Juma (32) na Juma Omary Hamis (28).

Kufikishwa mahakamani kwa washtakiwa hao kunatokana na mgogoro unaoendelea ndani ya chama hicho. Septemba 28, mwaka huu, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alitoa taarifa za kukamatwa kwa wafuasi hao kwa tuhuma za kupanga njama za kufanya fujo na kuchoma ofisi za CUF zilizopo Buguruni Ilala jijini Dar es Salaam.