SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 13 Oktoba 2016

T media news

Nje ya pitch – Mzee Akilimali ana hoja kuelekea mfumo mpya


Mzee Ibrahim Akilimali-Katibu Baraza la Wazee wa Yanga

Na Athumani Adam

“Mwaka 2006 tulikuwa na mgogoro kati ya Yanga asili na Yanga kampuni, tukafikia muafaka kwamba kuwe na Yanga SC pamoja na Yanga African Cooperation Limited ambayo itakuwa kampuni ya kusimamia hisa za Yanga”.

“Kipindi hicho bwana Yusuf Manji alikuwa mfadhili wetu, alihaidi kumnunulia kila mwanachama hisa kumi (10)”.

Hayo ni maneno ya mwanachama mkongwe wa Yanga, Mzee Ibrahim Akilimali alipotoa maoni yake kuhusu mchakato wa ukodishwaji wa klabu ya Yanga kupitia redio moja hapa nchini.

Kwa mujibu wa mzee Akilimali inaonekana Mwenyekiti Yusuf Manji, anaonekana kuja na mfumo mpya tofauti na ule ambao waliazimia miaka kumi iliyopita. Wana Yanga wanapaswa kuhoji hili, pia kujadili kwa kina upi ni mfumo sahihi kati ya ule wa mwaka 2006 na huu ambao unaonekana kuletwa na Mwenyekiti wao.

Bahati nzuri zipo klabu ambazo zinatumia mfumo kama ule ambao uliazimiwa na Yanga miaka kumi iliyopita ambao umebakia kwenye makaratasi.

Nchini Ujerumani kwenye jimbo la Westfalen ndani ya jiji la Dortmund, klabu maarufu ya Borussia Dortmund ni moja ya timu ambazo zinafuata mfumo ambao uliazimiwa na Yanga kipindi cha mgogoro.

Dortmund wana kampuni mbili, kampuni ya kwanza ni Borrusia Dortmund GmbH ambayo kazi yake kubwa ni kusimamia masuala yote yanayohusu timu. Pia kuna kampuni iitwayo Borrsusia Dortmund GmbH &KGaA yenye jukumu la kusimamia hisa za Borrusia Dortmund kwenye soko la hisa la Ujerumani.

Hii ni aina ya timu ambayo wanachama ndio wenye sauti juu ya maamuzi. Ina muundo wa uongozi ambao hautofautiani sana na klabu zetu za Simba na Yanga. Wamefanikiwa kupitia mfumo wa kuwa na kampuni mbili.

Wanasema kila kitu kina mwanzo, mfumo mpya wa uwekezaji kwenye mpira kwa staili ya kukodisha unataka uanzie Tanzania. Si Jambo baya wala sipo kwa kubeza kile kinachotakiwa kufanywa na Yanga, lakini je, wanachama wa Yanga wameangalia athari za kuiacha timu pamoja na masuala ya kibiashara yanayohusu timu kwa mkodishaji ambaye pia ni kiongozi wa klabu?

Manji atawezaje kusimamia maslahi yake pamoja na maslahi ya Yanga kwa wakati mmoja hali ya kuwa ndani ya klabu bado ni kiongozi mkuu? Kwa kuzuia mgongano wa maslahi ilikuwa sahihi Yanga ipate kionozi mwingine ambaye atasimamia maslahi ya Yanga na Mwenyekiti wa sasa abaki kwenye uwekezaji.

Yanga italazimika kufanyaka mabadiliko ya kikatiba, je ipi nafasi ya viongozi wengine ambao walichaguliwa sambamba na Manji kupitia mchaguzi mkuu? Kama kuna wajumbe waliweza kufukuzwa na Mwenyekiti hali ya kuwa wote walichaguliwa pamoja vipi wakiwa chini ya kampuni ya  Mwenyekiti.

Ipi nafasi ya wanachama katika kufanya maamuzi ya klabu baada ya mkodishwaji kupewa timu?

Kweli mpira unahitaji fedha, lakini sio kila fedha zinaweza kukupa kile unachotaka kukipata kwenye mpira. Kim Lee mfanyabiashara kutoka Asia alitaka kuinunua Liverpool ikashindikana, akaitaka AC Milan ikashindikana. Akaenda zake Valencia akafanikiwa kupewa timu.

Angalia ilivyo Valencia chini ya Kim Lee, wasikilize mashabiki wake wanavyolia na Lee pamoja na rafiki yake mkubwa, Mzee wa dili Jorge Mendes.