Na Baraka Mbolembole
LICHA ya kutolipwa mishahara yao kwa takribani miezi mitatu mfululizo, wachezaji wa Stand United wameendelea kufanya kazi yao uwanjani huku mkufunzi Mfaransa, Patric Liewig naye akiendelea kuwekeza mbinu zake kikosini na kuifanya timu hiyo ya Shinyanga kucheza game yao ya 8 msimu huu pasipo kupoteza katika ligi kuu ya kandanda Tanzania Bara (VPL).
Stand ililazimisha suluhu-tasa vs Mbeya City FC katika uwanja wa Sokoine, Mbeya siku ya Ijumaa hii na hivyo kufikisha alama 16 (pointi moja nyuma ya vinara Simba SC) katika msimamo. Ushindi ungewapeleka kileleni mwa msimamo lakini suluhu hiyo imewaacha katika nafasi ya pili.
Niliitazama game yao vs City, wachezaji wa Stand walicheza kwa malengo ya kusaka ushindi katika kipindi cha kwanza wakiongozwa na mzoefu, Amri Kiemba na walijilinda vizuri sana kama timu katika dakika 15 za mwisho baada ya City kuongeza kasi ili wapate matokeo katika uwanja wao wa nyumbani.
Kwa jinsi Stand ilivyocheza game hii usingedhani kama wachezaji wa timu hiyo wanadai mishahara ya miezi mitatu kama ilivyofichuliwa na mkufunzi Liewig mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo.
Kila mdau wa kandanda nchini anajua mgogoro wa kimaslahi ulivyo ndani ya timu hiyo hadi kupelekea wadhamini wa timu hiyo kampuni ya uchimbaji madini ya ACACIA kutangaza kujitoa kuendelea kuidhamini timu hiyo kabla ya kuanza kwa msimu huu.
Stand ilikuwa timu yenye udhamini mkubwa kuliko zote katika VPL lakini sasa Liewig amefichua wazi wachezaji wake wanacheza na kupata matokeo ndani ya uwanja lakini hawajalipwa mishahara yao kwa takribani miezi mitatu sasa.
Ni vyema viongozi wa timu hiyo wakawalipa sasa wachezaji wao ambao wengine inasemekana wanauguliwa na watu wao wa karibu lakini wanashindwa kutoa msaada kutokana na kutokuwa na chochote walichokipata kwa miezi mitatu sasa. Kiukweli, mimi ni kati ya mashabiki wakubwa wa Liewig tangu alipotua nchini kwa mara ya kwanza Desemba, 2012 katika klabu ya Simba SC.
Kocha huyo anajua kufundisha mpira huku akipendelea kujituma na kuwajibika kwa nidhamu kwa wachezaji wake.
Tangu ametua katika timu hiyo msimu uliopita, Liewig amefanya kazi kubwa na anapaswa kupongezwa kwa kuisaidia timu hiyo changa kutoka katika vita ya kuepuka kushuka daraja hadi kuwa timu yenye uhakika wa kubaki VPL.
Amekuwa akipigwa sana majungu ndani ya timu yake, baadhi ya wachezaji watovu wa nidhamu msimu uliopita na pia kuna wanachama na viongozi wa timu hiyo wamekuwa wakimpiga vita Liewig ndio maana walipanga kumtimua kama timu hiyo ingepoteza mchezo dhidi ya Yanga mwezi uliopita ambao walishinda 1-0.
Unawezaje kuandaa mikakati ya kumfuta kazi kocha ambaye timu yake haijapoteza mchezo katika ligi? Unawezaje kumfuta kazi kocha ambaye timu yake inajilinda na kushambulia vizuri?
Stand wameruhusu magoli matatu na kufunga magoli nane katika game zao 8 za msimu huu na ni timu mbili tu ambazo hazijapoteza mchezo katika VPL hadi sasa (Simba na Stand.)
Bado hawajachelewa sana, uongozi wa Stand United unapaswa kuwajibika sasa kuhakikisha wachezaji wao wanalipwa stahiki wanazodai. Wana kikosi kizuri ndani ya uwanja na kocha bora katika safu ya benchi la ufundi.
Mechi 8, Pointi 16, magoli 8 ya kufunga, magoli 3 ya kufungwa, Stand United walipeni wachezaji wenu mpate mafanikio zaidi.