SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 6 Oktoba 2016

T media news

Mayanga, Mandawa na urejeo wa Mtibwa Sugar katika mbio za ubingwa VPL

Na Baraka Mbolembole

RASHID Mandawa tayari amekwishafunga magoli matatu katika michezo 7 ya ligi kuu Tanzania bara msimu huu akiwa na kikosi cha Mtibwa Sugar FC ya Turiani, Morogoro.

Ni dalili nzuri kwa kikosi cha kocha Salum Mayanga ambaye amerejea katika timu hiyo akichukua nafasi ya ‘Mwanafunzi wake’ Mecky Mexime.

Mtibwa-mabingwa mara mbili mfululizo wa VPL miaka ya 1999 na 2000 imeanza ‘kukaa sawa’ baada ya kuwapoteza wachezaji wake wengi waliojiunga timu nyingine.

Golikipa, Hussein Shariff, mlinzi wa kati, Vicent Andrew, viungo Muzamir Yassin, Shiza Kichuya, Mohamed Ibrahim na mshambulizi, Said Bahanunzi wote walikuwapo katika kikosi cha timu hiyo msimu uliopita lakini sasa hawapo katika timu hiyo.

Pointi 13 katika game 7 zimeifanya timu hiyo kupanda hadi katika nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi-pointi nne nyuma ya vinara Simba SC.

Walipoteza mechi ya ufunguzi katika uwanja wao wa nyumbani, Manungu Complex kisha wakalazimishwa sare ya kufungana 1-1 na Mbao FC katika uwanja huo lakini mambo yameanza kwenda vizuri.

Goli pekee la kiungo mshambulizi, Haroun Chanongo vs African Lyon mwishoni mwa wiki iliyopita limekuwa goli la 8 kufungwa na kikosi cha Mayanga ambaye aliisaidia Tanzania Prisons kumaliza katika nafasi ya nne msimu uliopita huku wakicheza game 15 pasipo kupoteza katika uwanja wao wa nyumbani, Sokoine, Mbeya.

Wachezaji wengi wa Prisons walivutiwa na mbinu za Mayanga huku pia wakimsifia mkufunzi huyo wa zamani wa Kagera Sugar FC kwa kuwajenga kisaikolojia.

Mayanga amekuwa akiwasisitiza wachezaji wake mara kwa mara kwamba wanaweza kuifunga timu yoyote kama watakuwa tayari kwa maana mpira wao na timu nyingine hautofautiani. Chini ya kocha huyu naamini Mtibwa watajaribu kushinda ubingwa wa VPL na FA Cup msimu huu.

Akiwa tayari ameangusha pointi nne katika uwanja wa Manungu Complex na huku wakipoteza game moja ugenini vs Simba, Mayanga anapaswa kuimarisha zaidi mbinu zake za kujilinda ili wasiendelee kuruhusu magoli mara kwa mara.

Kuruhusu magoli 6 katika michezo 7 huku magoli matatu wakiruhusu katika uwanja wao wa nyu mbani ni tatizo lakini mkufunzi huyo naamini anaweza kurekebisha hali hiyo kabla ya kuwavaa JKT Ruvu ya Pwani pale Mlandizi wikendi hii.

Kushinda game nne, kupoteza mbili na kupata sare katika game moja ni mwanzo mzuri kwa timu iliyowapoteza wachezaji 6 hadi 7 wa kikosi cha kwanza kwa mara moja.

Nahodha msaidizi, Salim Mbonde, Ally Shomary, Ibrahim Jeba, na baadhi ya wachezaji wazoefu kama Vicent Barnabas na nahodha wa timu hiyo, Shaaban Nditti wanaweza kushirikiana na wachezaji vijana na wale wapya Kasian Mponela kumaliza tabia ya kumaliza ligi vibaya.

Mzunguko wa pili umekuwa ukiwasumbua sana Mtibwa katika miaka ya karibuni na jambo hilo limekuwa likiwanyima nafasi ya kutwaa ubingwa licha ya kufanya vyema mwanzoni na kutoa ushindani mkubwa.

Katika makocha wazawa, siku zote nimekuwa shabiki wa Mayanga-mshindi wa Tusker Cup 2008 akiwa na kikosi cha ‘Wakata Miwa hao wa Turiani.’

Mayanga atairudisha Mtibwa katika njia ya ushindani wa kweli na watajaribu kushinda mataji msimu huu. Mayanga anaweza kumaliza ‘kiu ya ubingwa’ Mtibwa Sugar lakini haitakuwa rahisi.